
WAZIRI wa Nishati, Medard Kalemani, ameagiza kukamatwa kwa maafisa wawili wa Kampuni ya Jumeme inayosambaza umeme wa jua kisiwani Maisome, Mwanza, kwa kuwauzia wananchi uniti moja ya umeme kwa TZS 3,500 badala ya TZS 100 na ameiagiza kampuni hiyo kurejesha fedha za wananchi huku akitoa onyo kali kwa wazalishaji binafsi wa umeme, wanaowatoza wananchi gharama kubwa tofauti na bei elekezi ya serikali.
Akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Kahunda, wilayani Sengerema, Mkoa wa Mwanza, Julai 7, 2020, alisisitiza kuwa gharama stahiki ya umeme kwa wananchi wote wenye matumizi ya kawaida ni shilingi 100 tu kwa uniti moja na kwamba wananchi wanapaswa kutozwa gharama inayofanana katika maeneo yote nchini kwani wote wana haki sawa.
“Bei hiyo ni kwa maeneo yote nchini vikiwemo visiwa na ni kwa umeme wa aina zote pasipo kujali ni wa TANESCO au kutoka kwa wazalishaji binafsi wanaotumia umeme jua na aina nyinginezo,” alisisitiza Dkt. Kalemani.
Alitoa agizo kwa viongozi wa serikali, hususan Wakuu wa Wilaya kote nchini, kuwachukulia hatua wazalishaji binafsi wa umeme, watakaobainika kukiuka mwongozo huo wa Serikali.
Alisema amekuwa akipokea malalamiko kutoka kwa wananchi mbalimbali, hususani wanaoishi visiwani, kwamba wamekuwa wakitozwa gharama kubwa na wawekezaji binafsi wa umeme hali inayosababisha wengi wajisikie kama wakimbizi ndani ya nchi yao.
Waziri alisema kamwe Serikali haitavumilia tabia za aina hiyo zinazoonyeshwa na baadhi ya wawekezaji binafsi wa umeme kwani imewaamini kutenda haki katika kuwafikishia umeme wananchi hao ambao hawajafikiwa na gridi ya Taifa.
Hata hivyo, alibainisha kuwa Serikali inaendelea na zoezi la kupeleka umeme wa gridi ya Taifa katika visiwa vyote nchini kwa kupitisha nyaya chini ya maji yanayozunguka visiwa hivyo. Aliwataka wananchi wa visiwani ambao hawajafikiwa na huduma hiyo kuwa watulivu kwani huduma hiyo itawafikia wote awamu kwa awamu.
Akiwa katika Mkutano huo, Waziri aliagiza kukamatwa na kuhojiwa wawakilishi wa kampuni ya kuzalisha umeme wa jua iitwayo Jumeme, baada ya wananchi wa Kisiwa cha Maisome wilayani humo, kuwatuhumu kuwa wamekuwa wakiwauzia umeme kwa gharama ya shilingi 3,500 kwa uniti moja.