×

Nusura Auawe na Wasiojuliana

MKAZI wa Kigogo Luhanga Mtaa wa Matokeo, Dar; Thadei Gregory (34), hivi karibuni alipoteza fahamu kwa wiki tatu bila kuzinduka baada ya kudaiwa kupigwa na wasiojulikana.

 

Akizungumza na mwandishi wetu Julai 2 mwaka huu, mke wa majeruhi huyo, Mwajuma Athumani, amesema tukio hilo lilitokea Mei 3 mwaka huu, baada ya mumewe huyo kutoka nyumbani wanapoishi kwenda dukani kupata mahitaji.

 

“Ilikuwa ni kama mkosi flani hivi, maana kama ningejua mume wangu anakwenda kufikwa na majanga yaliyompata, ni bora angebaki nyumbani nasi tulale na njaa kuliko balaa lililomkuta.

 

“Alipotoka tu, baada ya muda nikaona majirani zangu wananifuata nyumbani huku kila mmoja akianza kunihadithia kivyake tukio lililompata mume wangu.

“Taarifa hiyo ilinishtua sana, hivyo sikupata hata muda wa kuwasikiliza wamalize maneno yao, niliwauliza alipo na kumkimbilia nikamuone hali yake.

“Nilipofika nikamkuta mume wangu akivuja damu nyingi ambapo nilijaribu kumsemesha, lakini hakuweza kuzungumza chochote zaidi ya kuugulia maumivu.

“Tulikimbilia polisi kuchukua fomu ya matibabu (PF3), kisha tukamkimbiza hospitali ya jirani ili kumpatia huduma ya kwanza, lakini kutokana na hali yake, tulipewa rufaa kwenda Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

 

“Mume wangu alipelekwa ICU (Wodi ya wagonjwa mahututi), Kitengo cha Mifupa na Fahamu (MOI).

“Alilazwa wiki tatu bila kuzinduka ambapo wiki ya nne alizinduka na kutolewa wodi hiyo na kulazwa kwenye wodi ya kawaida lakini akiwa na tatizo la kumbukumbu.

 

“Mpaka hivi tunavyoongea, mume wangu hana kumbukumbu, mimi ananiita dada, mama yake mzazi anamuita mkewe.

“Yaani nimeingia kwenye ulimwengu mpya wa maisha magumu sana, maana mimi na wanangu pamoja na wazazi wake, wote tulikuwa tukiishi kwa kumtegemea yeye.

 

“Baada ya mkasa huo, tulifungua mashtaka polisi katika jalada lenye namba MBT/RB/1880/2020 ambapo waliomshambulia hawajapatikana, ingawa niliambiwa kuna mtuhumiwa mmoja alikamatwa lakini mimi sijui nini kinaendelea,” alisema mke wa majeruhi huyo.

 

Kufuatia sakata hilo, mwanahabari wetu alimtafuta mwenyekiti wa serikali ya mtaa huo, aliyejitambulisha kwa jina la Mfaume Mtikaliosi ambaye alikiri kutokea tukio hilo mtaani kwake.

“Hilo tukio nalifahamu, huyo majeruhi ni mwananchi wangu hapa mtaani na ingawa wakati tukio linatokea, sikuwepo lakini nilipata maelezo.

“Siku ya tukio kulikuwa na kikundi (sungusungu) kinamsaka mhalifu, sasa walisikia amejibanza maeneo ya karibu na anapoishi huyo majeruhi.

 

“Hivyo walipofika lile eneo, wakati wakiwa katika harakati za kumdhibiti huyo mhalifu, zilitokea kelele zilizokusanya watu ambapo miongoni mwa waliokusanyika kushuhudia tukio hilo, alikuwa Tadei.

“Katika hekaheka za kumkabili mtuhumiwa huyo, kuna jamaa alirusha kitu kama fimbo ambayo kwa bahati mbaya ilikwenda kumjeruhi Tadei kichwani.

 

“Baada ya mwananchi huyo kujeruhiwa, Wasamaria wema walimkimbiza hospitali ingawa ndugu wa familia hiyo walianza kuhamaki na kuniona mimi kama mwenyekiti wao sijawapa ushirikiano wa kutosha katika sakata hilo.

“Hata hivyo, pamoja na kunitupia lawama ya kutolichukulia umakini suala lao, nimekuwa nikienda kumjulia hali majeruhi huyo mara kadhaa na hivi karibuni niliwapelekea pole ya shilingi elfu hamsini, lakini bado naonekana mbaya.

 

“Unajua huku mtaani kwangu kila jambo watu wanataka kulifanya la kisiasa na hata hili kuna watu nafikiri wanakwenda kuishawishi ile familia hilo suala lilete sura mbaya kisiasa hapa mtaani,” alisema Mfaume.

MSAADA WAHITAJIKA

Kutokana na hali ya majeruhi kushindwa kurejesha fahamu zake ili aweze kuitunza familia na gharama za matibabu, msaada wa hali na mali unahitajika.

Endapo utakuwa umeguswa na mateso anayopitia Mtanzania mwenzako huyo, msaidie kupitia namba 0788 712 558, Jina Bahati Muanya.

RICHARD BUKOS, Risasi

Leave a Comment