×

Dkt. Mwigulu Nchemba Ashiriki Mkutano wa Afrika na Ufaransa Nairobi

WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba, leo Mei 12, 2026 ameshiriki katika ufunguzi wa Mkutano wa Ushirikiano kati ya Afrika na Ufaransa (Africa Forward: Africa–France Partnership for Innovation and Growth Summit) unaofanyika jijini Nairobi, Kenya.

Mkutano huo umewakutanisha Wakuu wa Nchi na Serikali, viongozi wa sekta binafsi, wadau wa maendeleo pamoja na wawekezaji kwa lengo la kuimarisha ushirikiano kati ya Afrika na Ufaransa katika sekta mbalimbali ikiwemo biashara, teknolojia, nishati, afya, Akili Unde (AI), kilimo, uchumi wa buluu pamoja na viwanda.

Akizungumza baada ya mkutano huo, Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba amesema mkutano huo umekuwa wa manufaa kwa Bara la Afrika na Ufaransa kwa pamoja kwani majadiliano yamegusa namna ya kuzifanya pande hizo mbili ziweze kunufaika na ushirikiano huo.

Amesema rasilimali zinazopatikana barani Afrika zinatosheleza ikiwa zitatumika vizuri katika kujenga uchumi wa Afrika.

“Lengo kubwa la jitihada hizi ni kupambana na umasikini lakini pia na kutengeneza ajira kwa makundi makubwa ikiwemo la vijana pamoja na wanawake,” amesema.


Akizungumza katika mkutano huo, Rais wa Jamhuri ya Kenya, Dkt. William Samoei Ruto, alizitaka nchi za Afrika kutafakari upya mifumo ya kiuchumi kwa kuimarisha ukusanyaji wa rasilimali za ndani, uwekezaji pamoja na ushirikiano wa kikanda ili kuhakikisha kunakuwa na maendeleo ya muda mrefu.

Kwa upande wake, Rais wa Jamhuri ya Ufaransa, Mheshimiwa Emmanuel Macron, alisema Bara la Afrika linapiga hatua kubwa za maendeleo na ni bara ambalo halisubiri majawabu ya changamoto bali linatoa majawabu ya changamoto mbalimbali lilazokabiliana nazo.

“Hatuko hapa tu kuja kuwekeza katika Bara la Afrika pamoja nanyi, tunawahitaji viongozi wakubwa wa biashara wa Afrika kuja kuwekeza nchini Ufaransa,” alisema.

MZEE LIPUTA MWENYE UPOFU na ANAYEMUUGUZA MKEWE APATA PIGO LINGINE – NYUMBA YOTE YADONDOKA…

Leave a Comment