×

Ifahamu Safari ya Lissu Kurejea Tanzania

LICHA ya Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu kutangaza tarehe ya kurudi Bongo, baadhi ya wachambuzi wa mambo ya kisiasa wamesema kuna shaka kama kweli anaweza kurejea nchini.

 

Wachambuzi hao waliozungumza na gazeti hili jana walisema Chadema awali kilitaka kihakikishiwe na Jeshi la Polisi usalama wa Lissu atakaporejea nchini, jambo ambalo hadi sasa hakuna taarifa za uhakika kuhusu hakikisho hilo.

 

Hivi karibuni Lissu alisema atarejea nchini kwamba itakuwa Julai 28, 2020 ili ahudhurie vikao vya juu vya chama vitakavyopitisha mgombea wa urais, ubunge na udiwani na yeye amejitokeza kuwania urais kupitia Chadema na kwamba tayari ameshakata tiketi ya ndege kurejea nchini.

 

Mmoja wa wachambuzi wa kisiasa, Abraham Kassim aliliambia gazeti hili kwamba ana shaka kama Tundu Lissu anaweza kurudi nyumbani kwa sababu amekuwa akisitisha mara kwa mara kurejea nchini kwa sababu alizodai kuwa za usalama wake.

 

“Mwaka jana Tundu Lissu ambaye alinusurika jaribio la kuuawa miaka mitatu iliyopita, aliwahi kusema mara kadhaa hadharani kwamba hayuko tayari kurudi nyumbani na ataendelea kubakia ughaibuni hadi pale atakapohakikishiwa na Serikali ya Tanzania usalama wake, anadai hajahakikishiwa, atarudije?” alihoji mchambuzi huyo.

 

“Lissu aliwahi kusema kwamba angerejea nchini Septemba 7 kuadhimisha siku aliyopigwa risasi na kuahidi kuwa angeshiriki kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa, lakini hakurudi, vipi leo tuamini kwamba atarudi mwisho wa mwezi huu?” alihoji.

 

Hata hivyo, baada ya ahadi hizo kutotimizwa na Lissu Chadema kilisema kinaafikiana na uamuzi wake wa kutorejea kikisema kuwa yale yaliyomkumba miaka mitatu iliyopita wakati akireja kwenye maskani yake akitokea katika vikao vya bunge bado ni tishio kwa sababu waliomshambuliwa hawajakamatwa.

 

Chama hicho kilisema jaribio la Lissu kurejea nyumbani kama alivyokuwa ameahidi hapo awali kuwa angerejea Septemba 7 mwaka jana zoezi lilisitishwa hasa baada ya kujitokeza baadhi ya watu wakimtishia kumdhuru wakati anaporejea nyumbani.

 

Mkurugenzi wa Itifaki, Uenezi, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema alisema ingawa mwanasiasa huyo haijulikani ni lini atarejea lakini alisisitiza kuwa suala la usalama wake ndiyo linalopewa kipaumbele kwa sasa.

 

Hata hivyo, Mkuu wa Jeshi la Polisi, (IGP) Simon Sirro aliwahi kukaririwa akisema kwamba usalama hapa nchini upo na alimtaka Lissu kurejea nchini bila shaka yoyote.

 

Tundu Lissu aliyevuliwa ubunge mwaka jana na Spika Job Ndugai, amekuwa akiishi nchini Ubelgiji tangu aliponusurika kifo baada ya kushaliwa kwa risasi na watu wasiojulikana Septemba 7 mwaka 2017. Aliwahi kusema ingawa sababu za kiafya za kuendelea kukaa nchini Ubelgiji haziko tena, lakini hakusudii kurejea nyumbani kwa sababu za kiusalama.

STORI | ELVAN STAMBULI, Risasi

Leave a Comment