
HOMA na hofu ya pambano la watani limepamba moto, ni baada ya Kocha Mkuu wa Simba Mbelgiji, Sven Vandenbroeck kuzuia shangwe za ubingwa wa Ligi Kuu Bara baada ya kuwazuia wachezaji wake kupanda kwenye gari kubwa maalum la wazi lililoandaliwa huku sababu ikitajwa ni Yanga.
Gari hilo lililofika kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar saa 2:05 asubuhi, liliandaliwa maalum kwa ajili ya wachezaji hao kupanda huku wakisherehekea ubingwa wa huo wa ligi waliouchukua kwa mara ya tatu mfululizo.

Msafara huo wa Simba ulitua kwenye uwanja wa ndege saa 3:00 asubuhi wakitokea Ruangwa, Lindi kabla ya kwenda kupanda ndege Mtwara na kuanza safari ya kurejea Dar wakitoka kucheza michezo yake miwili ya ligi na Ndanda FC, Namungo FC ambayo yote walimaliza kwa suluhu.
Baada ya kuwazuia wachezaji hao kupanda kwenye gari hilo, Sven akatoa maagizo wote wapande kwenye gari aina ya Toyota Coaster ya timu hiyo wanayoitumia U20 na ile ya wanawake.
Baadaye Sven alitoka kwenye mlango mkubwa wa kutokea abiria akiwa amekunja uso na kumfuata msaidizi wa Mtendaji Mkuu (C.E.O) wa timu hiyo, Senzo Mazingisa ambaye ni Rispa Hatibu kisha akamfuata ofisa mmoja wa Simba na kuanza kumfokea kwa sauti kubwa akisikika kuonekana kugomea mapokezi hayo.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata gazeti hili, kocha huyo kabla ya kuanza safari ya kurejea Dar, alizuia kuwepo mapokezi ya aina yake na badala yake kuwataka wachezaji wote kuingia kambini moja kwa moja baada ya kutua uwanja wa ndege.
Ilielezwa amefanya hivyo ili kutowachosha wachezaji wakati taya
ri wana mchezo mgumu mbele yao dhidi ya Yanga, keshokutwa Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa.
“Uongozi uliandaa gari maalum la wazi lililotolewa na Mo lililokuwa na matangazo mbalimbali ya bidhaa zake ambazo zinaidhamini timu hiyo, ndani ya gari hilo ulikuwepo muziki mkubwa ulioandaliwa kuwaburudisha wachezaji na mashabiki.
“Mara baada ya timu ilipofika mambo yakawa tofauti ni baada ya kocha kugomea mapokezi ya wachezaji waliokuwa wamebeba kombe hilo la ligi walilokabidhiwa Ruangwa.

“Kitendo hicho kimeonekana kuwakera viongozi hao walioongozana na msafara huo akiwemo Kaimu Rais wa Simba, Kaduguda (Mwina) ambaye yeye mara baada ya kumuona kocha anafoka, akaachana naye akaondoka na usafiri wake,” alisema mtoa taarifa huyo.
STORI NA WILBERT MOLANDI NA SAID ALLY,Dar es Salaam
Msafara wa timu hiyo ulianza safari ya kutoka uwanja wa ndege hapo saa 3:10 asubuhi kwa Toyota Coaster huku wakiliacha gari la wazi na kuelekea Mbweni Ndege Beach ambako timu hiyo imeweka kambi yake kujiandaa na mchezo dhidi ya Yanga.

Wakati wakifika kwenye hoteli waliyofikia basi la wachezaji lilingia mtaroni upande mmoja baada ya dereva kukosea mahesabu, mashabiki wakajitolea kulisukuma na kulinasua.
Katika mapokezi hayo maelfu ya mashabiki walijitokeza kuusindikiza msafara huo uliokuwa na bodaboda nyingi waliofika kuwasapoti wachezaji wa timu hiyo huku matawi kadhaa ya Mpira Pesa, Ubungo Terminal na Mpira na Maendeleo wakiongoza mapokezi hayo yalitumia saa mbili kufika kambini.