×

Washindi Wa Baba Lao Wasubiri Zawadi Zao Kwa Hamu Kubwa

WALE washindi saba waliopatikana kupita droo ya mwisho ya Bahati Nasibu ya Baba Lao au Jishindie Gari na Championi wamefunguka namna ambavyo wanasubiri kwa hamu kubwa kupewa zawadi zao.

 

Washindi hao waliongozwa na mshindi wa gari mpya aina ya Toyota FunCargo yenye thamani ya Sh milioni 10, Didas Marik mwenye miaka 42, ambaye aliibuka bingwa na kufanikiwa kujinyakulia ndinga hiyo ambayo anatarajia kukabidhiwa hivi punde.

Mbali na Marik ambaye ni mkazi wa Dar, wapo washindi wengine sita waliopatikana kupitia droo ndogo ambao ni Khalifa Mwipawa, Seleman Ally Ruzegea, Maulid Ally, Msafiri Mawila ambao wote ni wakazi wa Dar.

 

Wengine ni Mpoki Mwakyusa mkazi wa Mbeya na Kihiyo Hamisi mkazi wa TangaKwa nyakati tofauti washindi hao walikuwa wanawasiliana na Mkuu wa Idara ya Masoko na Usambazaji wa Global Publishers Anthony Adam, wakiwa na lengo la kutaka kujua lini watapewa haki yao hiyo.

 

Adam alisema washindi wamekuwa na shauku ya kutaka kupewa zawadi zao kutokana na kumsumbua mara kwa mara.“Washindi wamekuwa na shauku sana ya kupata zawadi zao ambazo bado tupo kwenye mchakato wa kuwakabidhi. Kimsingi ni haki yao kudai hizo zawadi na sisi tunazo, ila kuna utaratibu mdogo wa kiofisi bado haujakaa sawa.

 

“Kitu kikubwa ambacho kinatukwamisha ni suala la usajili wa gari, ambapo mchakato upo katika mamlaka ambazo zinahusika na kusajili, tukishakamilisha kuubadilisha usajili wa gari kwenda kwenye jina la Didas Marik, ndipo tutawaita wote na kuwapa haki yao,” alisema Anthony.

Championi lilitaka kujua lini washindi hao watapewa zawadi zao, Anthony alisema wanatarajia kutoa zawadi hizo mapema wiki ijayo kwa sababu kinachowakwamisha ni usajili wa gari la mshindi pekee, kwa kuwa fedha za washindi wengine sita zipo tayari na wanataka kutoa zawadi hizo kwa pamoja.

 

“Kiukweli, wiki ijayo mapema kabisa inaweza kuwa Jumatatu au Jumatano tunaweza kutoa zawadi hizo, usajili tu wa gari la mshindi ndiyo ambao unatukwamisha kwa sasa. Hatutaki kutoa zawadi kwa mafungu, tunahitaji kufanya kitu kikubwa kwa washindi wote.

 

“Kwa hiyo tunawaomba washindi wote wavumilie, tunafahamu wanahitaji sana kwa sasa kukamata zawadi zao ambao wamezipigania kwa zaidi ya miezi mitatu. Tunatoa ahadi kuwa wiki ijayo mambo yatakuwa mazuri na tutafanya hafla fupi ya shukrani kwa watu wote walioshiriki bahati nasibu hiyo,” alisema Anthony.

 

Droo ya bahati nasibu hiyo ilifanyika wiki iliyopita katika Viwanja vya Mabibo Sokoni jijini Dar na kushuhudiwa na mamia ya wakazi wa Jiji la Dar es salaam, huku timu ya Masoko na Usambazaji ya Global Publishers ikiwa inaendesha shughuli hiyo.

 

Naye Mwakilishi wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania, Elibariki Sengasenga alikuwepo eneo la tukio hilo kuhakikisha haki na utaratibu wa kuchezeshwa droo hiyo unafanikiwa pasipo kuvunja kanuni zinazoongoza michezo hiyo.

 

Wakazi mbalimbali waliojitokeza katika eneo hilo walipohojiwa na watangazaji wa +255Global Radio, Kissa Daniel na Gaby Mtanzania, walionyesha kufahamu uwepo wa bahati nasibu hiyo, huku wengine wakithibitisaha kuwahi kununua magazeti ya Championi na kushiriki bahati nasibu hiyo ila kwa bahati mbaya hawakubahatika kuwa washindi.Bahati nasibu hiyo ilianzishwa na Global Publishers kwa lengo la kurudisha kidogo kinachopatikana kwa jamii na watu wote ambao wamekuwa wakiisapoti Kampuni ya Global Publishers kwa zaidi ya miaka 20 sasa.

Stori: Issa Liponda, Dar es Salaam

Leave a Comment