×

Askofu Anglikana Aburuzwa Mahakamani kwa Tuhuma za Uzinzi

ASKOFU wa Kanisa la Anglikana, Visiwani Zanzibar; Michael Henry Hafidh, ameburuzwa Mahakama Kuu ya Vuga mjini humo, akikabiliwa na tuhuma za uzinzi.

Kesi hiyo Namba 21/2020 ilianza kutajwa mahakamani hapo Juni 29 mwaka huu mbele ya Mheshimiwa Jaji, Dkt. Yessaya Kayange.

 

Taarifa ambazo Risasi imezipata kutoka mahakamani hapo, zimeeleza kwamba tarehe tajwa, kesi hiyo ilitajwa na kisha kupangwa Julai 20, mwaka huu kuanza kusikilizwa.

Mlalamikaji mkuu katika kesi hiyo ya madai, ni Saburi Khamis mkazi wa Visiwani humo ambaye anamtuhumu askofu huyo kujihusisha kimapenzi na mkewe aitwaye Anun Ramadhani.

Saburi Khamis, mume aliyemburuza askofu mahakamani.

Akizungumza na mwandishi wetu, wakili wa mlalamikaji kutoka Chema Associate, amesema, askofu huyo anatuhumiwa kutenda kosa la Adultery (kufanya uzinzi na mke wa mtu huku akiwa anafahamu).

“Mteja wangu awali alikuwa na nia ya kukaa kikao cha usuluhishi na Askofu Hafidh, ili wayamalize nje ya mahakama, lakini ilishindikana.

“Basi ikatulazimu kukusanya vielelezo na kisha kumburuza mahakamani ambako ndiko inakopatikana haki.

Askofu Hafidhi.

“Naamini mahakama ndiyo itafanya kazi yake kwa weledi na kutoa haki kwa anayestahili,” alisema wakili huyo.

Aliongeza kwamba, kwa kuwa mteja wake ameathiriwa na tukio hilo, wamelazimika kumdai askofu huyo fidia ya shilingi milioni 100 kama atakutwa na hatia.

 

Risasi limefika mahakamani Vuga na kuona nyaraka mbalimbali za kesi hiyo zikiwa zimesheheni madai hayo mazito kwa askofu huyo ambapo kesi hiyo inatarajiwa kuanza kusikilizwa Julai 20 mwaka huu.

Timu ya waandishi wetu itaendelea kufuatilia kesi hii na kukuhabarisha msomaji hatua kwa hatua kupitia Magazeti Pendwa ya Global, Global TV Online na +255Global Radio.

STORI: MWANDISHI WETU, ZANZIBAR

Leave a Comment