Wezi nchini India wametoboa shimo kwenye treni iliyokuwa imebeba pesa na kuiba dola 750,000. Treni hiyo ilikuwa ikipita Kusini mwa India kuelekea Chennai safari ya kilomita 300 huku ikiwa na polisi waliokuwa wakilinda pesa hizo mali ya Benki Kuu ya India.
Hata hivyo walinzi hao waliokuwa ndani ya behewa lingine hawakusikia uhalifu huo ukitendeka na sasa wanachunguzwa. Treni hiyo ilikuwa imebeba dola milioni 51.
Polisi wanashuku kuwa kati ya wezi 6-8 walishiriki wizi huo kwa kutoboa shimo kwenye paa ya treni hiyo wakitumia kurunzi maalum ambayo hutoa miale yenye joto kali linayeyusha hata chuma bila ya kutoa kelele zozote.
Inspekta jenerali wa polisi M. Ramasubramani, amenukuliwa akisema ”Tunashuku walitoboa paa ya treni hiyo na wakaiba pesa hizo taslimu jumatatu usiku”
Wizi huo uligundulika jana Jumanne baada ya treni hiyo kufika mjini Chennai na wahudumu wakagundua kulikuwa na shimo na kisha kiasi cha fedha hizo zilikuwa hazipo.
Pesa hizo zilikuwa zimekusanywa ili ziharibiwe. Wizi huo umeibua kumbukumbu ya wizi uliotokea Uingereza mwaka wa 1963 almaarufu “Great Train Robbery” ambapo wezi walisimamisha treni na kuiba pauni milioni 2.6.
