×

Viongozi Yanga, ishikeni mkono Yanga Princess, kuna shida mahali

WIKI iliyopita ilikuwa ni wiki ya dabi za Kariakoo, ninapozungumzia dabi ya Kariakoo namaanisha kuwa mchezo wa soka ambao ulizikutanisha timu za Simba na Yanga.

Dabi hiyo ilianza siku ya Ijumaa kwa timu za wanawake za Simba na Yanga, kwa maana ya Simba Queens na Yanga Princess ambazo zilimenyana katika dimba la Uhuru ikiwa ni mwendelezo wa Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania Bara.

Mchezo ambao ulimalizika kwa Simba Queens kuwafunga Yanga Princess kwa mabao 5-1. Hii ni mara ya nne Simba wanakomba pointi tatu mbele ya Yanga, siyo pointi tatu tu, bali kwa vipigo vikali na fedheha, tunasema fedheha kwa sababu ikitajwa Yanga kila mmoja anaelewa inatajwa taasisi kubwa.

Msimu uliopita Yanga wakiwa wageni kwenye ligi hiyo, mechi ya kwanza walichapwa 7-0, mechi ya pili wakachapwa 5-1, wakati huo ilikuwa chini ya kocha Khamis Kihonda. Msimu huu timu ipo chini ya kocha pekee wa kike Tanzania Bara, Edna Lema (Morinyo). Mchezo wake wa kwanza dhidi ya Simba wakafa 3-1, kisha juzi wakafa 5-1.

Naamini utakuwa umeelewa tunaposema neno vipigo vya fedheha, kwa matokeo haya, Bodi ya Uhariri wa gazeti la Championi imehisi kuna shida mahali, shida yenyewe ni kwenye menejimenti. Viongozi wa Yanga wakiongozwa na Dkt Mshindo Msolla hawaipi thamani na kuijali hii timu kama inavyotakiwa.

Tunasema hivyo tukiwa na ushahidi wa macho, kwa sababu Championi limekuwa likifuatilia kwa ukaribu soka la wanawake, uongozi wa juu wa Yanga uonekana uwanjani mara chache sana, tena ikiwa timu hiyo inacheza na Simba, ndiyo utamuona Msolla au msemaji wa klabu hiyo, Hassan Bumbuli ama viongozi wa kawaida.

Yanga pia ni miongoni mwa timu ambazo zilichelewa kuingia kambini baada ya mapumziko ya Virusi vya Corona, hii pekee inatosha kusema kuwa viongozi hawapo serious na hii timu. Ukiwatazama Simba Queens kwa macho tu, utagundua kuwa wanapata huduma tofauti na ile ya timu nyingine kama Yanga.

Viongozi wa juu wa Simba wamekuwa wakionekana uwanjani mara kwa mara hata kama timu hiyo inacheza na kibonde Panama Girls. Mtu kama Hans Pope, Try Again na wengine wenye majina kwenye menejimenti ya Simba, wamekuwa wakihudhuria na kuongea na wachezaji kabla na baada ya mchezo.

Kuna mtu alitung’ata sikio kuwa, wale mabinti walipongezwa kwa dau la milioni 10 kwa kuwafunga tu Yanga. Maoni yetu kwenu viongozi wa Yanga, ishikeni na kuitazama hii timu ya wanawake kama mnavyoitazama ile ya wanaume.

Leave a Comment