×

Msuva Akataa ofa China, Aitaka Ligi ya Uingereza

KIUNGO mshambuliaji Mtanzania anayekipiga Klabu ya Difaa El Jadida ya nchini Morocco, Simon Msuva, amesema amepokea ofa nyingi na kati ya hizo ni kutoka China.

Nyota huyo wa zamani wa Azam FC, Moro United na Yanga, alijiunga na klabu hiyo mwaka 2017 akisaini mkataba wa miaka minne.

Akizungumza na Championi Jumatatu, Msuva alisema kuwa amekataa kujiunga na klabu za nchini humo kutokana na malengo aliyonayo ya kutaka kucheza soka la ushindani Uingereza.

Msuva alisema kuwa tayari ameanza kuwasiliana na baadhi ya mawakala mbalimbali aliowapa kibarua cha kumtafutia timu Uingereza.

Aliongeza kuwa ana matumaini makubwa ndani ya miezi miwili atakuwa ameshajua muafaka wake wa kubakia au kuondoka Difaa.

“Nimepata ofa nyingi kutoka kwenye baadhi ya nchi ikiwemo ya China ambayo hivi sasa imeendelea kisoka, ambazo nimezikataa kutokana na malengo yangu niliyojiwekea.

“Kikubwa malengo yangu ni kwenda kucheza soka la kiushindani Uingereza kama ilivyokuwa kwa Samatta, ninaamini ndoto zangu hizo zitatimia ndani ya miezi hii miwili.

“Tayari nimewapa kazi maalum baadhi ya mawala watakaonitafutia timu za kwenda kuzichezea, hivi sasa ninaendelea kujifua kwa ajili ya kujiweka fiti zaidi,” alisema Msuva.

WILBERT MOLANDI, Dar es Salaam

Leave a Comment