×

Aisha Masaka; Mtambo wa Mabao wa Tanzanite Queens Unaowesumbua Cosafa

JINA la Aisha Khamisi Masaka limekuwa likijijengea umaarufu kadiri siku zinavyozidi kusogea kunako ramani ya soka la wanawake Tanzania na Afrika. Ana miaka 17 uwezo wake upo katika kuzifumania nyavu kwenye kila mchezo anaocheza akiwa na jezi ya timu ya taifa.

 

Kwenye mashindano ya Cosafa yanayoendelea katika Jiji la Port Elizabeth nchini Afrika Kusini yalianza kutimua vumbi Novemba 3 na yatafikia ukomo Novemba 14, jina la Masaka limeshaingia kwenye kitabu cha kumbukumbu cha mashindano hayo hasa katika kuzifumania nyavu. Mashindano hayo ambayo yanashirikisha timu za wakubwa na zile za U-17, Tanzania imefanikiwa kupeleka timu mbili.

 

Tanzanite Queens (U-17) na ile ya wakubwa Twiga Stars. Twiga yenyewe imepangwa katika Kundi C pamoja na timu za Botswana na Zimbabwe, wakati Kundi A likiwa na timu nne, Afrika Kusini, Eswatini, Comoros na Angola.

 

Kundi B likiwa na timu tatu ambazo ni Malawi, Zambia na Lesotho na kufanya jumla ya timu kuwa 10 na timu nne ndizo zitafuzu kucheza nusu fainali. Huku kwa makinda wa U-17 kukiwa na timu nane, zikiwa katika makundi mawili A na B.

Tanzania wapo Kundi B na timu za Zambia, Comoros, Afrika Kusini na Lesotho, Kundi A ni Eswatini, Comoros, Afrika Kusini na Angola, wakicheza kwa mfumo wa ligi hadi fainali.

Jana Jumanne, Tanzanite Queens walikuwa na mchezo dhidi ya Zimbabwe ikiwa walishinda wataingia fainali kama wakipoteza idadi ya mabao na kadi itaangaliwa baina yao na Afrika Kusini kwa kuwa watakuwa wamelingana pointi.

Kwenye michezo mitatu, walishinda 5-1 mbele ya Comoro, wakachapwa 2-1 na Zambia, kisha wakawalaza 6-1 wenyeji Afrika Kusini.

Kwa upande wa Twiga Stars walicheza michezo miwili, wakishinda 1-0 dhidi ya Zimbabwe, wakichapwa 1-0 na Botswana. Matokeo hayo yanawafanya wakose nafasi ya kucheza nusu fainali kwa sababu Botswana waliwafunga Zimbabwe kwenye mchezo wa juzi Jumatatu.

 

Kwa kuwa kundi lao lina timu tatu yule mwenye pointi nyingi anakweda nusu fainali ambaye ni Botswana.

Sasa turudi kwa Masaka, mzaliwa wa Singida akicheza soka tangu akiwa shule ya msingi, kisha akalelewa na Alliance Girls na msimu huu wa Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania Bara Yanga Princess wamemsajili wakati wa dirisha kubwa.

 

REKODI ZAKE AKIWA COSAFA 2020

Ni kinara wa mabao na mchezaji aliyeweka rekodi ya kufumga mabao mengi zaidi kwenye mechi moja. Masaka amefunga mabao tisa katika michezo mitatu aliyocheza hadi sasa.

 

ALIFUNGA HAT-TRICK KWENYE MCHEZO WA UFUNGUZI

Wakiwachapa Comoros 5-1, akafunga bao moja wakati Tanzanite wakilala kwa mabao 2-1 mbele ya Zambia, kisha akaja akaweka chuma tano peke yake mbele ya Afrika Kusini, Tanzania wakishinda 6-1 na kuwa na hat-trick mbili kwenye mashindano hayo.

Wakati akiwa na kikosi cha Tanzanite Queens (U20), kilichotwaa ubingwa wa Cosafa mwaka jana mbele ya Zambia kwa ushindi wa 2-1, alimaliza mashindano akiwa amefunga mabao matatu.

 

YEYE NA HAT-TRICK

Tangu ameanza kucheza timu ya Taifa, Masaka amefunga jumla ya hat-trick nne kwenye michuno mitatu tofauti, kwa upande wa klabu amefunga hat-trick sita na kumfanya awe na jumla ya hat-trick 10 kwenye msimu wa 2018- 19 na 2019-20.

Amefunga hat trick mbili kwenye Cosafa ya mwaka huu, alifunga nyingine kwenye Cosafa ya U20 mwaka jana dhidi ya Eswatin, akafunga tena kwenye mashindano ya Cecafa yaliyofanyika mwaka jana nchini Uganda.

 

Kwenye Cosafa alifunga dhidi ya Djibouti, kisha akafunga nyingine mbele ya Burundi, kwenye michezo ya kufuzu Kombe la Dunia, michezo yote ikichezwa mwaja jana. Kwa upande wa klabu, alifunga dhidi ya Baobab Queens, Panama Queens na Mapinduzi Queens, hii ilikuwa ni 2018-19. Msimu wa 2019-20 alifunga dhidi ya JKT Queens, TSC Academy na Panama Queens.

MABAO MENGI KWENYE MECHI MOJA

Masaka akipata nafasi ya kufunga basi na atafunga kweli, aliweka rekodi ya kufunga mabao saba peke yake kwenye mashindano ya Cecafa, wakati wakiwaadhibu Djibouti kwa mabao 10-0.

 

MTAMBO WA KUZALISHA MABAO

Masaka amefunga mabao 30 katika michezo tisa aliyocheza akiwa na jezi ya timu ya taifa kati ya mwaka 2019- 2020, kiasi cha kuweka rekodi ya kuwa mchezaji kinda wa timu ya Taifa mwenye mabao mengi.

Championi lilipiga stori na Masaka ambapo alieleza haya kuhusu kasi yake ya kufunga: “Mimi kila ninapokuwa kwenye mashindano yoyote, lengo langu huwa ni kufunga mabao 100,” .

ISSA LIPONDA, Dar es Salaam

 

Leave a Comment