×

Farid Mussa Agomea Mkataba Tenerife, Arejea Bongo

KIUNGO mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Farid Mussa, amerejea nchini baada ya kugoma kuongeza mkataba mpya na timu ya CD Tenerife B ya nchini Hispania, baada ya kushindwa kufikia makubaliano ya kimkataba.

 

Farid amerejea nyumbani hivi karibuni baada ya mipaka ya kimataifa kufunguliwa tangu kutokea kwa janga la virusi vya Corona huku Hispania ikiwa ni moja ya nchi zilizoathirika vibaya kwa maambukizi na vifo vya watu wengi.

 

Akizungumza na Championi Jumatatu, Farid alisema kuwa amerejea nyumbani baada ya mkataba wake kumalizika huku akishindwa kufikia makubaliano ya kusaini mkataba mpya kutokana na kutofikia muafaka kwenye mkataba mpya.

 

“Nimerejea tangu mwezi uliopita kwa sababu kule mkataba wangu wa miaka minne umemalizika na sikuweza kuongeza mkataba mwingine, wenyewe walinitaka niongeze mkataba, baada ya ule wa awali kufikia kikomo, lakini niliweka kipengele kuwa lazima nicheze katika timu ya wakubwa na hapo ndipo lilikuwa tatizo kwao.

 

“Unajua huwezi kucheza ligi ambayo unashindwa kupata hata promo na ligi yenyewe wala haionyeshwi sehemu yoyote na watu kukuona hadi katika timu ya taifa jambo ambalo haliwezi kuwa salama kwangu lakini zimekuja ofa nyingi za kunitaka na wao wakaweka ngumu, nimerudi kujipanga kabla ya kufanya maamuzi,” alisema Farid.

IBRAHIM MUSSA, Dar es Salaam

Leave a Comment