
OFISA Habari wa Simba, Haji Sunday Manara, ameyanunua mabao yote yaliyofungwa katika mchezo wa watani wa jadi, Simba dhidi ya Yanga likiwemo la kiungo wa Yanga, Feisal Salum ‘Fei Toto’.
Katika mchezo huo wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam uliochezwa Jumapili iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa Dar, Simba iliibuka na ushindi wa mabao 4-1.
Wakati Fei Toto akiifungia Yanga bao hilo pekee, mabao ya Simba yalifungwa na Gerson Fraga, Clatous Chama, Luis Miquissone na Mzamiru Yassin.Manara alinunua kila bao kwa Sh 10,000 baada ya kukutana na mashabiki wawili wa Simba na Yanga ambapo alimpa Sh 40,000 shabiki wa Yanga aitwaye Yanga Kigelele, huku shabiki wa Simba, Said Simba akipewa Sh 10,000.
Manara alifanya hivyo jana Jumatano katika hafl a ya ugawaji wa zawadi kwa washindi wa shindano la Baba Lao lililoendeshwa na Kampuni ya Global Publishers kupitia magazeti yake ya michezo ya Championi na Spoti Xtra, huku yeye akipewa nafasi ya kutoa zawadi ya gari kwa mshindi aliyejishindia gari aina ya Toyota Fun Cargo.

Akizungumza na Spoti Xtra, Manara alisema: “Kutokana na ushindi tulioupata kwa watani zetu Yanga, kila bao nitalinunua kwa shilingi 10,000, hivyo nampa huyu mzee wa vigelele wa Yanga Sh 40,000 nikimaanisha elfu kumi ya kwanza ni bao la Fraga, ya pili Chama, ya tatu Miquissone na ya nne Mzamiru, huku huyu wa Simba nampa ya bao la Fei Toto.