
UNAWEZA kusema historia inajirudia Zanzibar baada ya Dk. Hussein Mwinyi kuibuka mshindi baada ya kupata asilimia 78 ya kura za wajumbe wa kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM na kuwapiku makada wengine wawili wa chama hicho akiwemo waziri kiongozi wa zamani wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar; Shamsi Vuai Nahodha.
Historia inajirudia kwa sababu Dk. Mwinyi ikiwa atachaguliwa kuwa rais wa Zanzibar, hiyo itakuwa mara ya pili kwa watoto wa marais visiwani humo kukalia kiti walichokalia wazazi wao, kwani wa kwanza alikuwa mtoto wa Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Shehe Abeid Karume; Dk. Amani Abeid Karume aliyekuwa rais kuanzia Novemba 8, 2000 hadi Novemba 3 2010.
Dk. Hussein Mwinyi, ni mtoto wa rais wa zamani wa Tanzania mzee Ali Hassan Mwinyi aliyekalia kiti hicho Januari 30, 1984 hadi Oktoba 24 1985.
Kutokana na uongozi wake uliotukuka; mzee Mwinyi, barabara moja muhimu jijini Dar es Salaam imepewa jina la Ali Hassan Mwinyi, pia uwanja wa mpira wa Tabora umepewa jina la Ali Hassan Mwinyi, shule nyingi nchini zimepewa jina lake.
Dk. Hussein Mwinyi alizaliwa Desemba 23 mwaka 1966 na kusomea Shule ya msingi Oysterbay, akamalizia Misri baada ya baba yake kuhamishiwa huko kikazi kama balozi na elimu ya sekondari aliipatia Shule ya sekondari ya Azania hadi kidato cha nne na Tambaza akamalizia kidato cha sita mwaka 1986 huku Tanzania Bara.
Elimu ya juu aliipata katika Chuo kikuu cha Marmara, Uturuki kuanzia mwaka 1986 hadi 1992 baadaye akapata shahada ya uzamivu ya utabibu wa kimataifa, Chuo kikuu cha Hammersmith Hospital, London, Uingereza mwaka 1993 hadi 1997.
Aliwahi kuwa mbunge wa Mkuranga, mkoani Pwani mwaka 2000 hadi 2005, lakini baadaye akawa Mbunge wa Kwahani Unguja mwaka 2005 hadi 2015 na sasa ni waziri wa ulinzi na jeshi la kujenga taifa alikotumikia kwa miaka kumi na moja.
Dk. Hussein Mwinyi amekuwa akibebeshwa wizara zinazowashinda wengine kwa sababu fulani fulani. Mwaka 2012 aliyekuwa Waziri wa Afya, Haji Mponda na naibu wake; Lucy Nkya, walipoondolewa kwa kushindwa kuwajibika, wakati huo Dk. Hussein alikuwa waziri wa ulinzi, akahamishiwa Wizara ya Afya.
Lakini pia mwaka 2013, Waziri wa Ulinzi, Vuai Nahodha, alipowajibishwa kutokana na kashfa ya utekelezaji wa Operesheni Tokomesa Ujangili, Dk. Hussein alikuwa Wizara ya Afya, alihamishiwa Wizara ya Ulinzi, hii inaonesha kuwa huyu anajua kazi na ndiyo maana akiishikilia wizara haikumbwi na kashfa nzito.
Baba yake mzee Ali Hassan Mwinyi alizaliwa Kivule, mkoani Pwani Mei 8, 1925, kama ilivyo kwa mwanaye naye aliwahi kuhudumu katika serikali zote mbili.
Mzee Mwinyi aliwahi kuwa waziri wa mambo ya ndani katika serikali ya muungano, ndiyo maana tunasema historia inajirudia, lakini pia aliwahi kuwa rais wa Zanzibar na baadaye rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Wakati wa kikao kilichofanyika mjini Dodoma mwishoni mwa wiki iliyopita na kuongozwa na mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi ambaye pia ni rais wa sasa wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli, Mwinyi alipata kura 129, na kuwashinda Nahodha na mwingine asiyefahamika sana Khalid Mohammed.
Dk. Hussein Mwinyi ametoa wito wa kuwepo mshikamano chamani kuelekea uchaguzi mkuu wa mwezi Oktoba ambao kihistoria upande wa Zanzibar huandamwa na upinzani mkali pamoja na vurugu.
Wagombea wengine walioshindwa wametoa ahadi ya kuunganisha nguvu ili kumwezesha Dk. Hussein Mwinyi kuchaguliwa kuwa rais awamu ya nane wa visiwa vya Zanzibar.
Katika hatua nyingine, kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM, pia kilimuidhinisha Rais John Magufuli kuwania kiti cha urais wa Tanzania na jina lake litapelekwa mbele ya mkutano mkuu wa chama uliofanyika kwa siku mbili na kupitisha kuwa mgombea urais wa Tanzania.
Rais Magufuli ambaye anawania muhula wa pili madarakani, amekuwa mwanachama pekee wa CCM aliyechukua fomu za kuwania kiti cha urais mwaka 2020.
Katika hatua nyingine, na kama inavyotazamwa na wengi kama njia ya kusaka umoja kuelekea kwenye uchaguzi mkuu, chama hicho kimemsamehe aliyekuwa katibu wake mkuu, Abdulrahman Kinana aliyekuwa amepewa adhabu kutokana na kile kilichoelezwa kuwa ni utovu wa nidhamu.
Wadadisi wa mambo ya siasa, wanasema Kinana atatumika katika kampeni za mwaka huu. Hata hivyo, chama hicho kimeendelea kumfungia milango, mwanasiasa wake, Bernard Membe aliyekuwa waziri wa mambo ya nchi za nje katika serikali iliyopita.
Membe ameachana na chama hicho na sasa amekuwa katika majadiliano na chama kimoja cha upinzani kwa shabaha ya kuwania urais.
MAKALA; ELVAN STAMBULI, UWAZI