
POLISI Mkoa wa Mbeya wanamshikilia dereva wa basi la Kampuni ya Kyela Express Denis Lameck (48) aliyekuwa akiendesha basi lenye namba za usajili T. 756 DEF aina ya Scania baada ya kusababisha ajali iliyoua mtu mmoja aitwaye Aida Iponja (42) mkazi wa Masukulu.
Kwa mujibu wa taarifa ya polisi, iliyotolewa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, Ulricho Matei, ajali hiyo imetokea juzi Julai 16, 2020 majira ya saa 22:20 usiku huko Kijiji cha Kyimbila kilichopo Kata ya Mpuguso, Tarafa ya Pakati, Wilaya ya Rungwe, Mkoa wa Mbeya katika barabara ya Tukuyu – Kyela ambapo basi hilo lilikuwa likitokea Dar es Salaam kuelekea Kyela liliacha njia na kupinduka na kusababisha kifo kwa abiria huyo.
Chanzo cha ajali ni mwendo kasi katika eneo lenye mkungu na mvua.
Aidha katika ajali hiyo abiria wanne walijeruhiwa ambao ni:-
Salome Shimti (43) Mkazi wa Kyela, Sabina Joseph (19) Mkazi wa Kyela, Talampe Kanyeye (41) Mkazi wa Kyela na Paschal Merimeri (36) Mkazi wa Jijini Mbeya.
Majeruhi wanaendelea na matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Rungwe Makandana na mwili wa marehemu umehifadhiwa Hospitalini hapo ambapo upelelezi zaidi unaendelea.
Wakati huohuo, polisi mkoani humo limesema linamshikilia Gwantwa Elias (30) mkazi wa Itunge, Wilayani Kyela, kwa kukutwa na pombe haramu ya moshi (gongo) yeny ujazo wa lita 100.
Mtuhumiwa amekamatwa Julai 16 huko Kijiji na Kata ya Itunge, Tarafa ya Unyakyusa, Wilaya ya Kyela, Mkoa wa Mbeya ambapo alifikishwa mahakamani Julai 17, 2020.