×

Flaviana Afichua Sababu za Kuja na Taulo za Kike

MISS Universe Tanzania 2007 ambaye kwa sasa ni mwanamitindo, mwanaharakati na mfanyabiashara maarufu, Flaviana Matata amesema alianzisha Lavy Sanitary Pads baada ya kuona wasichana wanavyopata tabu mashuleni wakati wa hedhi.

Flaviana alisema amekuwa akifanya kazi ya kuwahudumia wasichana wa kike kwa zaidi ya miaka 10 sasa, hivyo aliona namna ambavyo watoto wengi wa kike walikuwa wanakosa masomo wakiwa kwenye mzunguko wa hedhi, hali ambayo ilisababishwa na ukosefu wa taulo za kike (Pads) ambazo zingewasaidia kuendelea na ratiba ya masomo.

Flaviana aliyasema hayo kwenye kipindi cha Front Page kinachorushwa na +255Global Radio kila Jumatatu hadi Ijumaa, wakati alipofanya ziara katika Kampuni ya Global Publishers iliyopo Sinza Mori jijini Dar na kupata nafasi ya kusalimiana na timu ya Championi kabla ya kuelekea redioni.

 

Akizungumzia wazo la kuja na taulo hizo za kike Flaviana alisema: “Unajua nimekuwa nikifanya kazi za kuwahudumia wasichana kwa zaidi ya miaka 10 sasa kupitia taasisi yangu Flaviana Matata Foundation (FMF), hivyo najua mahitaji mengi ya wasichana hasa wale ambao wanaishi kwenye mazingira magumu, wapo ambao ukifika wakati wao wa hedhi wanashindwa kwenda shule kwa sababu ya kukosa taulo za kike.

“Hivyo nikapata wazo, miaka sita iliyopita kwamba lazima nije na kitu kama hiki, tukakutana na timu yangu, tukapanga na leo tumefanikiwa, tulitaka kuzigawa bure hizi taulo, lakini tukaona tukifanya hivyo tutashindwa kusogea kwa sababu huu ni uwekezaji, kwahiyo utakuwa tunauza, ila kila mwezi tutakuwa tunatoa taulo 100 bure kwa wasichana shuleni,” alisema Flaviana.

 

Mbali na hilo Flaviana aliwataka wasichana na wanawake wote kutoona hedhi kama jambo la siri sana, kwa sababu ni kitu cha kawaida kwa wanawake na kila mtu anafahamu hilo, hivyo ni vema wakawa wawazi kwenye changamoto zozote za hedhi ili waweze kupata msaada.

Stori: Issa Liponda,Dar es Salaam

Leave a Comment