
MAHAKAMA ya Wilaya ya Kigoma imemhukumu mkazi wa Katubuka Manispaa ya Kigoma/Ujiji, Jeremia Kilahunja (49), kifungo cha maisha jela kwa kubaka mwanafunzi wa shule ya msingi wa miaka mitano tangu akiwa na umri wa miaka sita.
Hukumu hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Katoki Mwakitalu, baada ya upande wa mashtaka kuthibitisha makosa matano yaliyokuwa yakimkabili.
Hakimu Mwakitalu alisema mahakama inatoa adhabu kali dhidi ya mshtakiwa huyo ili iwe fundisho kwake na kwa watu wengine wenye tabia kama hiyo.
Alisema upande wa mashtaka ukiongozwa na Wakili wa Serikali Raymond Kimbe, ulipeleka mahakamani mashahidi wanne na kielelezo kimoja cha PF3, ambavyo vilithibitisha kuwa mshtakiwa huyo alimbaka mwanafunzi huyo mara tano.
Kadhalika, alisema siku ya tukio mwanafunzi huyo alikuwa akirudi kutoka shuleni na kumkuta mshtakiwa akipalilia shamba karibu na nyumbani kwao na alipomwona alimwita na kumwomba akamnunulie chakula ndipo mwanafunzi huyo alipoenda nyumbani na kubadilisha nguo na kumfuata mshtakiwa ili akachukue pesa ya kununua chakula hicho.
Alisema baada ya mwanafunzi huyo kuondoka, mshtakiwa alimuita na kumwambia kuna kitu amesahau na aliporudi alimkamata na kumpeleka kwenye vichaka na kumwamuru avue nguo na kuanza kumbaka huku akimtishia kumcharanga panga kama atamwambia mtu kuhusu tukio hilo.
Mwakitalu alisema mshtakiwa huyo mara ya kwanza alimbaka mwanafunzi huyo akiwa na umri wa miaka sita mwaka 2015, mara ya pili mwaka 2016, mara ya tatu mwaka 2017, mara ya nne mwaka 2018 na mara ya tano mwaka 2019.
Alisema mara ya tano mshtakiwa alimkuta mwanafunzi huyo akiwa na mdogo wake wanachunga mbuzi maeneo ya Airport, alimwita na kumpeleka vichakani na kuanza kumbaka. Mdogo wake aliyekuwa naye alikuwa akiwachungulia na mbakaji alipomaliza kufanya tukio hilo la kinyama, watoto hao walirudi nyumbani.
Hakimu alisema, walipofika nyumbani mdogo wa mwanafunzi huyo alimwambia mama yake tukio lililotokea wakati wakiwa wanachunga.
Alisema mama yake alimchukua mtoto wake hadi kituo cha polisi na kupewa PF3 kwa uchunguzi na daktari alithibitisha mwanafunzi huyo hakuwa na bikira na ilionekana kufanyiwa kitendo kwa muda mrefu.
Hakimu Mwakitalu alisema upande wa mashtaka umethibitisha makosa yote matano na kumtia hatiani kwa makosa yote.
Hakimu Mwakitalu alitoa adhabu kwa kosa la kwanza kwenda jela maisha, kosa la pili a jela maisha, kosa la tatu jela maisha, kosa la nne jela maisha na kosa la tano jela miaka 30, lakini makosa yote yanakwenda pamoja hivyo atatumikia kifungo cha maisha jela.
Awali, akisoma hati ya mashtaka Wakili wa Serikali Raymond Kimbe, alidai tarehe isiyofahamika mwaka 2015 eneo la Airport Manispaa ya Kigoma/Ujiji, mshtakiwa alimbaka mwanafunzi akiwa na umri wa miaka sita. Tarehe isiyofahamika mwaka 2016 alimbaka tena mwanafunzi huyo akiwa na umri wa miaka saba. Tarehe isiyofahamika mwaka 2017 maeneo ya Katubuka mshtakiwa alimbaka mwanafunzi huyo akiwa na miaka minane.
Pia, tarehe isiyofahamika mwaka 2018 maeneo ya Katubuka mshtakiwa alimbaka mwanafunzi huyo akiwa na miaka sita na mwaka 2019 maeneo ya Jusi, mshtakiwa alimbaka mwanafunzi huyo akiwa na miaka 10 kinyume cha sheria.