
MTIA nia wa ubunge kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Jimbo la Kawe, ambaye pia ni msanii na mtangazaji wa runinga, Mwijaku Burton, amewanyooshea vidole baadhi ya wajumbe wa mkutano mkuu wa Jimbo hilo (CCM) akidai kuwa wamekuwa wakichaguana kwa kujuana ndiyo maana jimbo hilo limeendelea kuwa mikononi mwa wapinzani.
Mwijaku ametoa kauli hiyo leo Jumanne, Julai 21, 2020, wakati akinadi sera zake na kuomba ridhaa ili achaguliwe na kupitishwa na chama hicho kupeperusha bendera yake katika uchaguzi wa mbunge jimbo la Kawe huku akiwataka wasifanye kama walivyofanya jana wajumbe wa CCM Kigamboni.
Wajumbe wa CCM Kigamboni walimpa kura nyingi za ndiyo aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo, Dkt. Faustine Ndugulile, ambaye alipata ushindi wa kura 190 dhidi ya aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, aliyepata kura 122.
“Tuache unafiki, jimbo la Kawe ni gumu, mkiendelea kuchaguana kwa tabia zilezile, ni pagumu hapa, mmewachagua wengi na mmeona wametuangusha.
“Sasa huu ni wakati wa kufanya maamuzi makavu live; tunaenda kulirudisha jimbo hili,” amesema.