×

Uchaguzi Mkuu 2020: Ni Vita ya Magufuli vs Membe

Mchezo wa mpira wa miguu ndio mchezo unaopendwa zaidi duniani ikilinganishwa na michezo mingine kama vile mpira wa wavu, kikapu au ndondi.

Katika mchezo huo, mashabiki hujaa uwanjani pindi timu pinzani zinapovaana hususani zile timu ambazo ni watani wa jadi. Kwa maana ya kuwa ni timu zenye historia inayoshabihiana lakini pia ni timu zenye mashabiki wengi ikilinganishwa na timu nyingine kama ilivyo kwa Yanga iliyoanzishwa mwaka 1935 na Simba mwaka1936.

Unapofika wakati wa mechi, timu hizo ambazo huwa ni wapinzani wa jadi, huibua msisimko wa aina yake kwa kuwavutia mashabiki ambao hujazana uwanjani ili kushuhudia mechi hiyo ambayo kila upande kuanzia mashabiki, benchi la ufundi hadi wachezaji hutamba kushinda.

Vivyo hivyo katika siasa, tumeshuhudia viongozi wenye historia zinazokaribia kushabihiana pindi wanapovaana mpambano wake huwa wa kukata na shoka.

Mwaka 2015 tulishuhudia mpambano wa aina hiyo ambapo viongozi wenye sifa zilizoshahibiana Dk. John Magufuli na Edward Lowassa waliamsha ari ya Watanzania kushiriki uchaguzi huo kutokana na historia ya makada hao.

Kwamba walikuwa ni wanachama wa CCM, wameitumikia Serikali iliyoongozwa na chama hicho kwa nyakati tofauti kabla ya Lowassa kukatisha safari yake ya matumaini ndani ya CCM na kuhamia Chadema kabla ya kurejea tena CCM akijia kwamba hawezi tena kugombea urais.

‘KACHERO’ KUNOGESHA UCHAGUZI?

Mbio za Uchaguzi Mkuu mwaka huu nazo zimeanza kunoga. Kama alivyobainisha ‘kachero mbobezi’ Bernad Membe kuwa kete yake ndio itakayonogesha uchaguzi huo, na sasa ni dhahiri kuwa baada ya kutegua kitendawili na kuweka bayana mwelekeo wake kisiasa, sasa uchaguzi umeanza kuchangamka.

Membe ambaye alifukuzwa mwezi huu na Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC) licha ya kuwa tayari amerejesha kadi yake ya uanachama, anatarajiwa kuleta ushindani wa kipekee kati yake na Rais John Magufuli ambaye anatetea ungwe ya pili ya uongozi wake.

Tayari Membe amechukua fomu ya kuwania kuteuliwa kuwa mgombea urais wa Chama cha ACT Wazalendo huku akipewa nafasi kubwa ndani ya  chama ambacho kimeonekana kushika hatamu kwa upande wa upinzani.

Hata hivyo, Membe ambaye alikuwa pia waziri wa mambo ya nje katika kipindi ambacho Rais John Magufuli alikuwa waziri wa ujenzi na wizara nyingine alizoshika kipindi cha uongozi wa awamu ya nne chini ya Rais Jakaya Kikwete, anatarajiwa kuleta ushindani kutokana na wawili hao kuwa na historia zinazoshabihiana.

Mwanadiplomasia huyo anatajwa kuleta ushindani kutokana na makundi yaliyopo CCM yanayodaiwa kumuunga mkono ilihali hayajitokezi hadharani.

Aidha, Membe ndiye anayetajwa zaidi kutoa upinzani huo kutokana na msukumo mkubwa wa kumsimamisha mgombea mmoja kutoka upinzani, ikilinganishwa na mgombea kutoka Chadema ambapo Tundu Lissu ndiye anayepigiwa chapuo zaidi ikilinganishwa na wagombea wengine.

NI ZAMU YA KURA KUMWANGUKIA MTU AU CHAMA

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ruaha, Profesa Gaudence Mpangala anasema ni dhahiri kuwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, watu wanaelekea kufanya uchaguzi kwa kuzingatia sifa, uweledi, uzalendo na ufanisi wa mtu na sio chama kama ilivyokuwa mwaka 2015.

Hoja hiyo ya Prof. Mpangala inatokana na ukweli kuwa mwaka 2015, Chadema kilibebwa na wakereketwa wa mabadiliko, kwa mantiki hiyo ndio maana walipata kura nyingi kutoka kwa wananchi waliochagua chama na sio mtu.

Wapo baadhi ya wananchi wamelieleza UWAZI kuwa katika uchaguzi huo  walipofika katika chumba cha kupigia kura, licha ya kwamba hawakumtambua mgombea udiwani wala ubunge, lakini wakamchagua kwa sababu tu ni upinzani au kwa sababu ni CCM.

“Zilikuwa kura za hasira ikilinganishwa na mwaka huu, sasa watu wametulia, wamefanya tathmini na wataamua kwa kupiga kura kwa kuangalia aina ya mtu wanayempigia, kuwa amewafanyia nini, amekuwa mtetezi wao kivipi, haya ni mambo ambayo yanaweza kujitokeza katika uchaguzi huu,” anasema Dk. George Kahangwa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

…KETE YA UPINZANI KUUNGANA MUHIMU

Profesa Gaudence Mpangala anaongeza kuwa licha ya kwamba Watanzania wengi wanamtazama Membe kuwa mshindani kindakindaki kwa Magufuli, bado wasisahau kuwa Chadema hawajatangaza mgombea wao. Vilevile bado haijafahamika kuwa mgombea wa Chadema ambacho ni chama kikuu cha upinzani iwapo atakuwa ni Freema Mbowe, Lazaro Nyalandu au Tundu Lissu anayepigiwa chapuo zaidi.

“Kwa upande wa upinzani, wakiweka wagombea wawili wenye nguvu maana yake kura za upinzani wataipa faida CCM kupita kwa urahisi katika uchaguzi huo, wakiweka mmoja kwa kukubaliana kuwa atakuwa Membe au Lissu hapo ushindani wa kweli utadhihirika lakini wakigawanyika huku Membe kule Lissu alafu Magufuli katikati, basi wapinzani wameumia.

Aidha, Prof. Mpangala anaonya kuwa ikumbukwe katika uchaguzi wa 2015 ulikuwa na ushindani mkubwa kati ya Magufuli na Lowassa, pia matarajio ya wapinzani ni kwamba Chadema wangeshinda uchaguzi huo ndio maana makada wengi wa CCM wakahamia Chadema.

“Lakini cha kushangaza CCM ilipita. Ilipitaje hatujui ila chama kilichopo madarakani kinakuwa na uwezekano zaidi wa kushinda ndio maana makada wengi wa upinzani wanakimbilia CCM.

“Labda kutokee uchaguzi huru na haki jambo ambalo kwa vyama tawala vya Afrika sio rahisi kuruhusu uchaguzi wa aina hiyo. Mara nyingi chama kilichopo madarakani kinatumia mbinu mbalimbali kwa kupitia dola kushinda uchaguzi,” anasema.

Hata hivyo, mjadala huo wa kusimamisha mgombea mmoja wa upinzani umekwishapigiwa chapuo pia na Membe mwenyewe ambaye kabla na baada ya kuhamia ACT Wazalendo, alisisitiza umuhimu wa vyama vya upinzani kumsimamisha mgombea mmoja.

Hili ni jambo linalosubiriwa kwa hamu na Watanzania wengi ili kupata ladha ya uchaguzi wenyewe ambao umenogeshwa na mafahali wawili waliokuwa zizi moja hapo awali kabla ya kuingia ulingoni.

NA GABRIEL MUSHI

Leave a Comment