×

Mbelgiji Atimua Mastaa 13 Yanga SC

KOCHA Mkuu wa Yanga, Luc Eymael ameshakamilisha ripoti yake licha ya kubakia vitu vichache lakini amesisitiza ndani ya ripoti hiyo lipo la kuwaondoa wachezaji 13 wakiwemo wa kigeni.

Ripoti hiyo imesisitiza kuwaondoa mastaa wote wakigeni ambao wamekuwa na mchango mdogo ndani ya timu hiyo na kupelekea kushindwa kufanya vizuri katika Ligi Kuu Bara na Kombe la FA Yanga kwa sasa ina wachezaji tisa wa kigeni ambao ni kipa Mkenya, Farouk Shikhalo, Wanyarwanda, Patrick Sibomana na Haruna Niyonzima, Mzambia, Eric Kabamba, David Molinga na Papy Tshishimbi wote raia wa DR Congo, Mghana, Lamine Moro na Bernard Morrison na Gnamien Yikpe raia Ivory Coast.

Eymael, ameliambia Championi Jumatano kuwa amepanga kuwaondoa wachezaji 13 wakiwemo wa kigeni kwa kuwa anataka kujenga timu itakayokuwa na ushindani mkubwa huku akipanga kusajili wachezaji wapya kati ya tisa hadi kumi kwa ajili ya msimu ujao.

 

“Ripoti imeshakamilika kuna mambo machache nataka kuyamalizia baada ya ligi kuisha kabla ya kurejea nyumbani kupumzika, ila nimepanga kuacha wachezaji 13 ili nijenge timu imara kwa msimu ujao.“Kiukweli siyo wengi hao kwa sababu nataka kujenga timu imara maana huwezi kuwa na mchezaji wa kimataifa halafu anazidiwa uwezo na mchezaji wa ndani hao kwangu hawatokuwa na nafasi.

“Nataka kuwa na wachezaji wa kimataifa ambao watakuwa na msaada kwenye timu wengi wataondoka, nitasajili wachezaji tisa hadi kumi ili kuleta ushindani wa kweli,” alisema Eymael.

 

Inaelezwa kuwa baadhi ya wachezaji ambao watapigwa chini licha ya kutotajwa ni Shikhalo,Molinga,Sibomana, Kabamba,Yikpe,Morrison kwa wageni huku baadhi ya wachezaji wa ndani ni Mrisho Ngassa, Ramadhan Kabwili, Andrew Vincent, Paul Godfery,Raphael Daud.

Stori: Ibrahim Mussa na Abdulghafal Ally

Leave a Comment