×

Wazee 15 wa ‘Nitumie kwa Namba Hii’ Wanaswa – Video

WAKAZI 15 wa Wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashitaka mbalimbali ikiwemo kula njama, kutenda kosa la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kutumia laini za simu za watu wengine bila kutoa taarifa.

 

Washitakiwa wamesomewa mashitaka yao mbele ya mahakimu tofauti akiwemo Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Saidi, Rashid Chaungu, Augustina Mbando, Yusto Ruboroga na Richard Kabate.

 

Washitakiwa hao ni Meniad Ndiyo (25), Mkulima, Dereva Boda boda, Dotto Likumbai (29) , Abdallah Migoi (26) mkulima na Mawakala wawili ambao ni Athumani Roho (28) na Onesmo Ngajela (24).

 

Pia wengine ni Saidi Sevenjari maarufu Dangote (35) mkulima na Hasani Njalatango 34 mkulima, Filbert Ngatunga (26), Octavian Lekaleka (26) mfanyabiashara Francis Mhombera (24), Moses Mhindi (25) dereva bodaboda, Michael Ngalami (21) na Omary Mbena (31) Wakala.

 

Washitakiwa wengine ni Rashid Mshamu (23) ambaye ni dereva pikipiki na Emmanuel Assey (19) ni Wakala.

Miongoni mwa mashitaka waliyosomewa washitakiwa hao wanadaiwa kati ya Januari Mosi na Juni 15, 2020 maeneo mbalimbali wilayani Kilombero Mkoa wa Morogoro kwa pamoja walikula njama kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

 

Pia mshtakiwa Sevenjari, kupitia ujumbe mfupi wa maandishi inadaiwa alituma ujumbe ukisema “Umepokea Sh 300,000 kutoka kwa Antony Ngonyani mnamo Juni 22 mwaka huu saa mbili asubuhi salio 750,000.

 

Dangote anadaiwa alijipatia Sh 2,132,980 kutoka namba mbalimbali kwa kudanganya kwamba fedha hizo zimetumwa kimakosa arudishiwe.


Pia wanadaiwa kushindwa kutoa taarifa ya mabadiliko ya laini ya simu kosa walilolitenda, Januari Mosi na Juni 15 mwaka huu maeneo mbalimbali ya Kilombero, walitumia namba za simu zilizosajiliwa kwa majina ya watu wengine bila kutoa taarifa kwa mtoa huduma.

 

Inadaiwa walilitenda kosa hilo kati ya Januari 1 na Juni 15, 2020 Kilombero mkoani Morogoro ambapo walikuwa njama ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

 

Pia wanadaiwa kuchapisha taarifa za uongo ambapo wanadaiwa kulitenda Aprili 15, 2020 Ifakara Morogoro ambapo walituma ujumbe kwa mfumo wa Kompyuta wakisema “Imethibitishwa umepokea 170,000″ kutoka kwa Adamson Cheyo na kusema salio lako ni 430,000”

 

Kosa jingine ni kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu ambapo wanadaiwa kulitenda Januari 1 na Juni 15, 2020 katika maeneo tofauti mkoani Morogoro ambapo kwa nia ovu walijipatia Sh. Milioni TATU wakidai fedha hizo zimetumwa kwa watu kimakosa.

 

Katika mashitaka ya kusambaza ujumbe wa kielektroniki inadaiwa Ndiu, Likumbai, Migoi walianzisha ujumbe wa mtandao kuonesha Ashura Birika amepokea Sh 150,000 Aprili Mosi, 2020 saa 3:03 asubuhi na salio lake ni Sh 230,000.

 

Washitakiwa walikana mashitaka na washitakiwa walirudishwa rumande kwa kushindwa kutimiza masharti ya dhamana, huku baadhi ya mashitaka upelelezi ukiwa umekamilika. Kesi zimeahirishwa hadi Julai 27, Agosti 5 na 6, 2020.

Leave a Comment