×

Kusah: Mimi na Aunt Acha Lizame!

WE umenikaa, umenikaa kwa roho…

Nafsi mpaka akili yangu…

We dada umenibamba mmmh mhh…

Ooh darling, halafu tumetokaga mbali mmh…

Sioni dalili ya kukuumiza ukalia…

Halafu darling, mwenzako nakupenda kweli…

Tufike wawili, sitaki mwingine kwa safari…

Penzi letu lime-takeover…

Nimekunywa, nina hangover…

Umegeuka gari, umenigonga mmmh mhh…

Penzi letu lime-takeover…

Nimekunywa, nina hangover…

Umegeuka gari, umenigonga…

Umenishika kichwa, umeninyonga…

Ila kelele lele, wana kelele lele…

Kelele lele, wana kelele lele…

Ooh kelele lele (maneno ya kando kando)…

Wana kelele lele (hawanaga mipango)…

Kelele lele (yatakwisha baba)…

Wana kelele lele (iye iye iye)…”

Hii ni sehemu ya mashairi yenye hisia kali kunako Ngoma ya Kelele ya mkali mwingine wa Bongo Fleva, Kusah akimshirikisha mzazi mwenzake, Ruby.

Jina halisi la Kusah ni Salmin Issa.

Mbali na Kelele, jamaa amesikika sana kwenye mapini mengine makali kama Chelewa. Ya Dunia, Angalau, Dakika, Pandisha, Nilikudanganya, Mkongo, Sakata, Wema, Sijawahi Pendwa na Hujanikomoa. Kwa sasa anatamba na mkwaju mpya unaokwenda kwa jina la Pole.

Zipo stori nyingi kitaani kwamba, kama siyo Ruby, huyu mwamba angekuwa bado anasaga soli bila kutoka, kwani kolabo nyingi alizofanya naye akiwa tayari yupo kwenye ramani, ndizo zimemtoa.

Hata hivyo, analaumiwa kwa kumzalisha na kumtema Ruby ikielezwa kuwa, huko ni kukosa shukrani.

Lakini sasa, Kusah anatengeneza vichwa vya habari akidaiwa kuwa kwenye uhusiano shatashata wa kimapenzi na staa wa Bongo Movies, Aunt Ezekiel ambaye ni mzazi mwenza wa dansa wa Wasafi, Moze Iyobo.

Stori za Kusah na Aunt zinakwenda mbali zaidi ikidaiwa kuwa, tayari mwanamama huyo amebeba ujauzito.

OVER ZE WEEKEND huwa haiwezi kukaa na ukakasi kooni, hivyo imetafuta mzani kwa kukaa kitako na Kusah kwenye mahojiano maalum (exclusive) akiwa mkoani Iringa alikokwenda kumsindikiza mwigizaji wa Bongo Movies, Steven Mengere ‘Steve Nyerere’ kuchukua fomu ya ubunge.

Kusah amefunguka mengi juu ya uhusiano wake na Aunt;

OVER ZE WEEKEND: Mambo vipi Kusah?

KUSAH: Poa kabisa, maisha yanasonga.

OVER ZE WEEKEND: Hongera nimesikiliza ngoma yako ya Pole ni nzuri na inafanya poa…

KUSAH: Asante sana. Mungu anasaidia, tunajitahidi hivyohivyo.

OVER ZE WEEKEND: Pole ni moja ya ngoma zako ambazo Aunt anapenda kusikiliza na hata kuimba na kuposti kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii. Kwa nini Aunt anafanya hivyo kwako na siyo mwanamuziki mwingine?

KUSAH: Ninachokijua Aunt ni shabiki wangu na anapenda sana muziki wangu, ndiyo maana unaona anaziposti.

OVER ZE WEEKEND: Lakini inasemekana wewe na Aunt mpo kwenye uhusiano wa kimapenzi na tayari Aunt ni mama kijacho, hii ishu imekaaje?

KUSAH: Hata mimi naona watu wanaandika hivyohivyo kwenye mitandao ya kijamii na hata watu wanaongea, lakini mimi ninachojua Aunt ni dada mzuri na mwenye moyo safi.

OVER ZE WEEKEND: Kwa nini sasa iwe ni wewe na siyo mwanamuziki mwingine?

KUSAH: Inawezekana kwa sababu anapenda kusapoti nyimbo zangu, lakini hata hivyo watu wakumbuke Aunt ni singo na mimi ni singo, inawezekana Mungu akaleta heri huko mbele, kwa hiyo acha lizame!

OVER ZE WEEKEND: Kutokana na tetesi hizo za kutoka kimapenzi na Aunt na inafahamika miezi michache alikuwa kwenye uhusiano na Moze Iyobo. Je, hiyo haikupi shida kuwa karibu naye?

KUSAH: Hakuna tatizo lolote na hata kama ingekuwa kweli, sidhani kama Aunt ana mtu na hata tulivyojuana tu kawaida, alikuwa peke yake, hivyo sina shaka na lolote.

OVER ZE WEEKEND: Vipi kuhusu Ruby na yeye kwa upande wake hajakuletea shida kwa sababu ni mzazi mwenzako?

KUSAH: Hapana. Kwanza Ruby ni mzazi mwenzangu tu na tumebaki kuwa hivyo. Hatuna uhusiano mwingine wowote zaidi ya kulea mtoto wetu.

OVER ZE WEEKEND: Kwa hiyo wewe na Ruby huwa mnakutana kwa ajili ya mtoto wenu?

KUSAH: Kiukweli sijakutana naye kwa muda mrefu, lakini kuna njia tunatumia kuwasiliana kwa ajili ya mtoto wetu.

OVER ZE WEEKEND: Vipi kuhusu muziki wako unakulipa?

KUSAH: Si unajua hapa kwetu Bongo, bado tunajikongoja. Lakini mimi pia ni mtunzi na nimewaandikia wanamuziki wengi nchini Kenya, hivyo angalau maisha yanateleza.

OVER ZE WEEKEND: Kuna ugumu wowote unaoupata kwenye muziki wako?

KUSAH: Ugumu upo sana, lakini tunapigana, naamini tutafika tu, cha msingi ni kutokukata tamaa.

OVER ZE WEEKEND: Umefanya ngoma kadhaa ukiwa na Ruby na hasa Ngoma ya Kelele ambayo ilifanya na inaendelea kufanya vizuri, je, una mpango wa kufanya tena kolabo na yeye?

KUSAH: Yule ni mzazi mwenzangu. Kama ikitokea chansi nitafanya kwa sababu najua kitakachopatikana ni kwa ajili ya mtoto wetu.

MAKALA: IMELDA MTEMA, IRINGA

Leave a Comment