
KATIKA Parokia ya Mtakatifu Imakulata Kanisa Katoliki Upanga jijini Dar es Salaam alipokuwa anasali, Rais Mstaafu Benjamin Mkapa, ameacha alama ya unyenyekevu na kutopenda kujikweza.

Hayo yamebainishwa na Paroko wa parokia hiyo, Padri Casmir Kavishe alipozungumza na HabariLEO ofisini kwake jana mara baada ya Misa ya Kwanza kumalizika.

Padri Kavishe alisema Mkapa alipenda atambulike kama muumini wa kawaida kama walivyo waumini wengine kanisani hapo na hakutaka cheo chake cha ‘Mheshimiwa Rais Mstaafu’ kitumike katika kumtambulisha au kumuita.
“Mkapa alikuwa muumini mzuri na mcha Mungu, kila Jumapili alikuja kanisani na asipoonekana kanisani ilikuwa ama amesafiri au mgonjwa. Alikuwa anawahi kanisani, hakupenda kujikweza, alikuwa mnyenyekevu, alikuwa anakuja na watu wachache kanisani na siyo rahisi kujua kama yupo kanisani,”alisema Padri Kavishe.



