
MAKAMU Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino, Profesa Costa Mahalu, amesema kifo cha Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, ni pigo kwa taifa lakini kipekee, akimkumbuka zaidi kwa kumuokoa kwenda jela bada ya kumtolea ushahidi mahakamani.
Akimzungumzia Mkapa, Profesa Mahalu alisema zaidi atamkumbuka kutokana na ukaribu wao wawili wa muda mrefu ambapo alisimama naye katika mambo mbalimbali hadi kwenda kumtolea ushahidi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu alipokuwa ameshitakiwa kwa kuhusika na ununuzi wa jengo la Ubalozi wa Tanzania nchini Italia.
Alisema alimfahamu Mkapa tangu Mwaka 1988 walipokutana kwa mara ya kwanza Geneva, Uswizi, akitoka katika mkutano wa kisheria ambapo kwa wakati huo Mkapa alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje na kuanzisha urafiki, suala alilokuwa amelifurahia hasa baada ya kusikia mambo mazuri aliyokuwa akiyafanya siyo kwa Tanzania tu, bali Afrika na dunia kwa ujumla.

Alisema mwaka 1992 alipoteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Elimu ya Juu, Mkapa aliteuliwa kuwa Waziri wa Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia na kudai kuwa kwa muda wote alipofanya naye kazi aligundua kuwa Mkapa alikuwa kiongozi msikivu aliyekuwa na tabia ya kumsikiliza kila mtu, jambo lililomfanya apendwe na watu wengi.
“Tulinunua jengo zuri sana na baadaye lilikuja kuleta matatizo, kama mnavyofahamu, na hata nilivyokuja kumueleza alinipa moyo kwa kuniambia kuwa suala hilo litakwisha, tulijenga undugu sana na mimi kumuona kama kaka yangu.
“Mzee Mkapa alikuwa na mtizamo mzuri na mwalimu wangu kisiasa, hata alipoitwa mahakamani alikuja na kunisaidia kwa kuwa alikuwa ni mtu asiyependa uonevu,” alisema.
Mahalu aliongeza kusema kamba Mkapa alikuwa mtu wa kupenda uwazi na ukweli, hakupenda majungu na kwa kuwa alikuwa akifahamu undani wa ununuzi wa lile jengo, hivyo hakuona shida kwenda mahakamani kumtetea.

Alisema baada ya utetezi ule uliomfanya kushinda kesi mahakamani, yeye na familia yake walikwenda kanisani na kumshukuru Mungu na kuongeza kuwa kifo chake kimemhuzunisha sana, akiamini kuwa siku moja atakutanishwa naye tena.
SOMA: Mkapa afichua sababu ya kumtetea Prof. Mahalu
Rais mstaafu Benjamin Mkapa ameeleza sababu iliyomfanya kuamua kusimama mahakamani kumtetea aliyekuwa balozi wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Mahalu.
Mkapa aliongoza nchi kuanzia mwaka 1995, wakati wa uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi tangu siasa za ushindani zirejeshwe mwaka 1992, hadi mwaka 2005 alipomkabidhi Jakaya Kikwete.
Profesa Mahalu na Grace Martin aliyekuwa ofisa utawala wa ubalozi huo, walishtakiwa mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakidaiwa kuisababishia Serikali hasara ya Euro 2,065,827.60 (Sh5 bilioni) katika mchakato wa ununuzi wa jengo la ubalozi nchini Italia.
Katika kitabu chake cha “My Life, My Purpose (Maisha Yangu, Kusudi Langu)” , Mkapa anasema alichukua uamuzi huo kwa kuwa alikuwa anafahamu ukweli wa jambo hilo lilitokea chini ya utawala wake.
“Mimi ndiyo nilitoa idhini ya kufanya malipo kwa utaratibu huo baada ya kupewa maelezo na Profesa Mahalu, ambaye kutokana na mwenye jengo kusisitiza utaratibu huo kwani lilikuwa jambo la kawaida nchini Italia,” anasema Mkapa katika kitabu hicho.
Mkapa anasema tuhuma dhidi ya Mahalu zilitolewa katika mazingira ya kutatanisha kwa kuwa kuna mtu alipiga simu katika redio moja na kudai alikuwa ana ushahidi wa tuhuma dhidi ya Profesa Mahalu na ndiyo maana Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ikaanza kuchunguza.
Mkapa anaeleza kuwa alifanya jitihada za kuwaona Takukuru ili kuwaomba waachane na kesi hiyo kwa kuwa hakukuwa na tatizo na malipo hayo, lakini waliamua kuendelea nayo.
Alisema kutokana na hali hiyo ndipo alipokata shauri na kuamua kupanda kizimbani kwa nia ya kumtetea Mahalu.
“Nilishangaza wengi kwa uamuzi wangu wa kwenda mahakamani kumtetea Profesa Mahalu. Ninaelezwa hata Rais Jakaya Kikwete hakuamini pale aliposikia kuwa ninakwenda mahakamani,” anasema Mkapa.
Mkapa na msafara wake ulioongozwa na maofisa wa itifaki, aliwasili mahakamani kutoa ushahidi wake siku hiyo.
Alikula kiapo maalumu katika kesi hiyo iliyosikilizwa na Hakimu Mkazi Mfawidhi, Ilvin Mugeta, ikiongozwa na Alex Mgongolwa, mmoja wa mawakili wa Profesa Mahalu.
Mkapa alijibu maswali kwa kujiamini na kwa umakini mkubwa huku mara kadhaa akiwavunja mbavu wasikilizaji kwa jinsi alivyowajibu mawakili wa Serikali.
Mkapa alisema kuwa Serikali yake ilifahamu ununuzi wa jengo hilo na taratibu za malipo baada ya kufahamishwa na Profesa Mahalu na kwamba lilinunuliwa kwa maagizo ya Serikali yake.
SOMA: Rais Magufuli Amrejeshea Prof. Mahalu Hadhi ya Ubalozi
March 18, 2018, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John Magufuli alimresjeshea Prof. Costa Mahalu hadhi yake ya ubalozi ikiwa ni miaka takribani 11 tangu avuliwe hadhi hiyo.
Prof. Mahalu alivuliwa hadhi ya ubalozi mwaka 2007 baada ya kufunguliwa mashtaka ya jinai na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hata hivyo, mwaka 2012, mahakama ilitoa hukumu kwamba Prof. Mahalu hakuwa na hatia.
Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya nje ilisema “Kuanzia leo tarehe 17/3/2018, Prof. Mahalu ataendelea kuwa na heshima ya kuitwa balozi.”