
PAZIA la Ligi Kuu Bara kwa msimu wa 2019/20 jana lilimalizwa kibabe kwa klabu za Ndanda FC ya Mtwara, Alliance ya Mwanza na Lipuli FC ya Iringa kuiaga ligi hiyo baada ya kushuka daraja.
Klabu hizo zimeungana na Singida United kukamilisha seti ya timu nne ambazo zimeshuka daraja na kuangukia Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kwa msimu ujao ikiwa ni kanuni iliyopitishwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ya kupunguza timu kutoka 20 hadi 18 msimu ujao.
Lipuli wakiwa kwao Iringa katika Uwanja wa Samora, walichapwa bao 1-0 na Yanga huku Ndanda wakipoteza kwa mabao 2-0 mbele ya Mbao FC kwenye Uwanja wa CCM Kirumba. Licha ya ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Namungo FC, haikuwapa faida Alliance ya kubakia kwenye ligi hiyo baada ya kuzidiwa mabao ya kufunga na kufungwa dhidi ya ndugu zao Mbao FC.
Katika hatua nyingine timu za Mbeya City ya Mbeya na Mbao FC zitaenda kucheza michezo ya mtoano ‘playoff’ dhidi ya Geita Gold na Ihefu FC.
Mbeya City watacheza dhidi ya Geita Gold kutoka Kundi B ya FDL, nyumbani na ugenini, kisha itakayoibuka kidedea itacheza Ligi Kuu Bara msimu ujao.
Mbao watacheza na Ihefu SC ya Mbeya mechi mbili za mtoano, mshindi wa jumla atacheza ligi kuu msimu ujao.
Licha ya kuwa na mwendo wa kusuasua Yanga wamefanikiwa kumaliza nyuma ya mabingwa Simba wakiwa na pointi 72 baada ya kushinda mbele ya Lipuli wakiwapiku Azam FC waliomaliza wa tatu na pointi 70 baada ya kutoa sare ya mabao 2-2 na Tanzania Prisons mjini Mbeya.
Wakati vita hiyo ya kupanda na kushuka ikishika hatamu, mshambuliaji wa Simba, Meddie Kagere kwa mara ya pili mfululizo amefanikiwa kuibuka mfungaji bora baada ya kumaliza na mabao 22.
Kagere amechukua tuzo hiyo akiwaacha mbali Waziri Jr wa Mbao na Yusuph Mhilu wa Kagera ambao wamefunga mabao 13 kila mmoja.
MSIMAMO BARA
P W D L F A GD Pts
1. Simba 38 27 7 4 78 21 57 88
2. Yanga 38 19 15 4 45 28 17 72
3. Azam 38 20 10 8 52 26 26 70
4. Namungo 38 17 13 8 46 37 9 64
5. Polisi TZ 38 15 10 13 37 35 2 55
6. JKT 38 13 15 10 34 32 2 54
7. Coastal 38 14 11 13 33 30 3 53
8. Kagera 38 15 7 16 44 41 3 52
9. Biashara 38 12 14 12 29 27 2 50
10. Prisons 38 10 19 9 35 30 5 49
12. Mwadui 38 12 11 15 39 45 -6 47
12. Ruvu 38 12 11 15 34 42 -8 47
13. KMC 38 13 7 18 35 46 -11 46
14. Mtibwa 38 11 12 15 30 34 -4 45
15. Mbeya 38 12 9 17 33 42 -9 45
16. Mbao 38 12 9 17 33 43 -10 45
17. Alliance 38 11 12 15 36 48 -12 45
18. Lipuli 38 12 8 18 43 51 -8 44
19. Ndanda 38 9 14 15 28 35 -7 41
20. Singida 38 4 6 28 23 73 -50 18.
WAANDISHI WETU | Dar es Salaam