×

Mwijaku Kortini kwa Tuhuma za Kusambaza Picha za Utupu

MTANGAZAJI na msanii, Mwemba Burton maarufu Mwijaku (35) amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Jijini Dar es Salaam, leo Jumatano, Julai 29, 2020, akikabiliwa na mashitaka ya kusambaza picha za utupu.

 

Mwijaku ambaye alikuwa mmoja wa watia nia jimbo la ubunge la Kawe, amefikishwa mahakamani hapo leo, Julai 29, 2020 na kusomewa shtaka lake mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Richard Kabate.

 

Akisoma shtaka hilo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon, akisaidiana na Mwanaamina Kombakono, alidai kuwa mshtakiwa anakabiliwa na kesi ya jinai namba 110.

Wakili Kombakono alidai mshtakiwa alitenda kosa hilo, kati ya Septemba 15, 2019 na Oktoba 10, 2019 katika jiji la Dar es Salaam. Alidai katika kipindi hicho, Mwijaku alichapisha picha za ngono kupitia mtandao wa kijamii wa WhatsApp aliouunganisha katika kompyuta.

 

Mshtakiwa amekana shtaka na amekosa dhamana baada ya kushindwa kutimiza masharti ambayo ni kuwa na wadhamini wawili kutoka ama Bongo Movie au tasnia ya muziki wenye barua zilizothibitishwa na Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA), ambao watasaini bondi ya Sh  500,000 kila mmoja.

 

Hakimu Kabate ameahirisha kesi hiyo hadi Agosti 12, 2020 itakapotajwa.

Leave a Comment