×

Mwinyi: Mungu Msamehe Mkapa, Nilibeba Viatu Begani – Video

RAIS mstaafu wa awamu ya pili wa Tanzania, Alhaji Ali Hassan Mwinyi, amemwomba Mwenyezi Mungu kumsamehe Hayati Benjamin William Mkapa pale alipoteleza wakati wa uhai wake.

 

Akizungumza baada ya kupewa nafasi hiyo na Rais John Magufuli wakati wa kutoa salamu za mwisho kijijini Lupaso, Mtwara, Mwinyi amesema, Mkapa naye ni mtu hivyo kuna mahali  aliteleza.

 

“Ndugu yetu marehemu Mkapa ni mwanadamu kama walivyo wengine, labda katika maisha yake aliwahi kufanya kosa asilolipenda muumba wetu. Katika hali kama hii, mwenzetu akiondoka, jambo la kwanza ni kumuombea usalama kwa Mwenyezi Mungu endapo kakosea. Kaanza kukosa baba yetu Bwana Adam, basi kama ana kosa, Mwenyezi Mungu amsamehe,” amesema.

 

Mwinyi ametoa pole kwa Mama Anna, Mjane wa Mkapa, ndugu na jamaa kutokana na msiba huo, akisema miongoni mwa mambo anayokumbuka kutoka kwa Mzee Mkapa nikutokuwa na mchezo kazini.

 

“Nafsi yangu kama zilivyo nafsi zenu imegubikwa na huzuni kwa kuondokewa na ndugu yetu, Kaka yetu, mwenzetu Mkapa, katika hali kama hii muhimu ni kumuombea mwenzetu kama ana makosa Mungu amuwie radhi, Mkapa alikuwa mtu mwema sana na mfanyakazi kwelikweli.

 

“Leo hii nasimama hapa kutoa rambirambi kwa Mama Mkapa, na kwa watu wote wa Mkoa huu, kwa kuondokewa na rafiki mpenzi, Marehemu Mkapa alikuwa ni mtu mzuri sana, mwema sana, lakini mfanyakazi kwelikweli hana masihara katika kazi.

 

“Kwa kweli nafsi yangu kama zilivyo zenu zimegubikwa na huzuni, kwa kutuondokea ndugu yetu Mheshimiwa Mkapa, katika hafla kama hii mwanadamu yanamuishia ya kusema hata kama akiwa na neno.

 

Hata hivyo, Mzee Mwinyi amesema, kwenye shughuli hiyo kuna jambo amelikumbuka katika miaka ya nyuma, hata kama wengine wanaweza kuliona dogo.

 

“Mimi ndiye mtu mkubwa kuliko wote hapa. Nimezaliwa mwaka 1925, mnaweza kuona ni jambo dogo, lakini kuna jambo ambalo nimeliona hapa. Nyinyi nyote mmevaa viatu, mimi nilivaa viatu mara mbili, mara ya kwanza nilipokwenda jandoni nikiwa na miaka 13 na mara ya pili nilipovuna karafuu nikapata hela nikanunua viatu, nilikuwa navivua naweka begani visiishe,” kauli hii ilimfanya Rais Magufuli na wengine kuangua kicheko.

 

Leave a Comment