KAMATA Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) imewapitisha Tundu Antipas Lissu, Lazaro Nyalandu na Dr Mayrose Majinge, kusaka nafasi ya kuwania urais Tanzania.
Katika kikao chake cha Kamati Kuu kilichomalizika usiku mnene majina hayo jana jioni yalipelekwa ndani ya Baraza Kuu ambao watakata ‘mzizi wa fitna’ kumpata mgombea mmoja baada ya kupigiwa kura na jina moja kuwasilisha ndani ya Mkutano Mkuu leo kuidhinishwa.
Yeyote atakayepitishwa na Baraza Kuu atakuwa anafaa kuwania urais kama atatimiza vigezo vilivyowekwa na kuchambuliwa na chama hicho.
Matokeo ya kura za Baraza Kuu yamempa ushindi Tundu Antipass Lissu kwa asilimia 91% ambapo jina lake leo litapelekwa kwenye Mkutano Mkuu kuidhinishwa.

Jumla ya wapigakura 442
Hakuna kura iliyoharibika
1. Tundu Lissu kura 405
2. Lazaro Nyalandu kura 36
3. Dkt. Mayrose Majinge kura 1.
Aidha, Salum Mwalimu amependekezwa kuwa Mgombea-Mwenza wa Urais Tanzania kwa kura 451 za ‘Ndiyo’ kati ya 456. Leo jina lake litapelekwa kwenye Mkutano Mkuu kuthibitishwa.
Mara baada ya kutangazwa matokeo ukumbi ulilipuka kwa shangwe huku Lazaro Nyalandu akiahidi Baraza Kuu kumuunga mkono Tundu Lissu kwa asilimia zote.
Aidha, Baraza Kuu la Chadema limempendekeza kwa Mkutano Mkuu wa chama hicho, Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Zanzibar), Said Issa Mohamed kuwa mgombea Urais wa Zanzibar.