×

Baba Aua Binti Yake kwa Kipigo, Anaswa Akimzika kwa Siri!

BWANA mmoja aliyetambulika kwa jina la Maurice Owino Owaga (48) mkazi wa Muhoroni, Kisumu nchini Kenya, anashikiliwa na polisi kwa kosa la kumpiga binti yake wa miaka 15 na kumsababishia kifo. Mtu huyo alikamatwa akiwa anajiandaa kumzika kwa siri.

 

Inadaiwa kwamba, baba huyo alimpiga binti yake kwa kosa la kutoka nyumbani kwenda kulala kusikojulikana bila kuwa na idhini yake. Owaga alikamatwa na kupelekwa katika kituo cha polisi cha Chemelil baada ya kunaswa aking’ang’ana kuuzika mwili wa binti wake.

 

Taarifa zinadai kuwa, mshukiwa amekuwa akimpatia marehemu kichapo cha mbwa kila mara na hata hadi kifo chake alikuwa anauguza majeraha mengine ya kipigo. Aidha binti yake mwingine wa miaka 14, yuko hoi baada ya kupigwa na baba yake huyo. Binti aliyefariki alikuwa ni darasa la saba.

 

Akithibitisha kisa hicho, Kaimu Kamanda wa Kaunti ya Kisumu, Erick Wanyonyi, Owaga atafikishwa mahakamani na atashtakiwa kwa kosa la mauaji. Wanyonyi amewataka wazazi kuwa makini hasa wanapowaadhibu watoto wao msimu huu ambao wamo kwenye likizo ndefu.

 

Leave a Comment