×

SMART CODES Kuwapiga Msasa Wanafunzi Wabunifu Vyuo Vikuu

Mkurugenzi Mtendaji na mwanzilishi wa Smart Codes, Edwin Bruno (kushoto) akiwa na Meneja mradi, Sharron Nsule.

Kampuni ya Smart Codes kupitia Jukwaa la Smart Lab pamoja na  Taasisi ya Human Development Innovation Fund (HDIF), imeandaa programu maalumu ya mafunzo kwa wanafunzi 400 vyuo vikuu nchini yenye lengo la kuwajengea uwezo wa kuwa wabunifu kiteknolojia na kuwawezesha kupata ajira kwa urahisi.

 

Programu hiyo imeandaliwa kwa wanafunzi hao kutoka vyuo vikuu nchini ambavyo ni Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo Kikuu cha St. Joseph, Taasisi ya Teknolojia ya Dar es salaam (DIT) na Taasisi ya Fedha na Usimamizi (IFM).

 

Akifafanua kuhusu programu hiyo, Mkurugenzi Mtendaji na mwanzilishi wa Smart Codes, Edwin Bruno alisema kwa kuzingatia fursa zilizopo kwenye mabadiliko ya teknolojia, wanaamini kuna nafasi nzuri katika kukuza talanta za wajasiriamali vijana wenye akili ya ubunifu.

 

Alisema Smart Lab inakusudia kuhakikisha kuwa programu hii inafanikiwa na kuleta matokeo yanayoweza kupimika na yanayoonekana hata baada ya kukamilika.

 

“Programu hiyo itatolewa njia ya mtandaoni kwa wanafunzi hao ili kuwajengea uwezo katika maeneo muhimu zaidi ili kupata ajira na pia kuwafanya kuelewa namna ya kuwa wavumbuzi wenye uwezo wa kutoa suluhisho katika matatizo yaliyoko kwenye jamii yetu.

 

“Pia itatoa nafasi kwa wanafunzi kufikiria juu ya shida zinazowazunguka, kuunda suluhisho za ubunifu na kukuza mawazo ya biashara karibu na suluhisho hizi.

 

“Programu hiyo itahusisha shughuli mbalimbali kama vile mafunzo ya ufundi stadi, warsha za namna ya kutengeneza bidhaa za kiteknolojia ambazo zinajumuisha ushirika wa pamoja katika makampuni ya kiteknolojia,” alisema

 

Alisema Smart Lab pia imeshirikiana na kampuni kadhaa na inatarajia kushirikiana na nyingine zaidi ili kuwawezesha wajasiriamali kuibua vipaji vyao zaidi.

 

“Smart Lab na HDIF inawakaribisha vijana wote wenye kiu ya kujifunza, kujiandikisha kwa ajili ya kuwa sehemu ya program hii. Hii itakuwa nafasi nzuri ya kujifunza na kutambua uwezo wao kama vijana. Pia utakuwa mwanzo wa kuelewa kazi zao na kuchagua njia sahihi ya ukuaji wao katika kile wanachokibuni.

 

“Tunadhamiria kuwawezesha vijana na kuwaunganisha na makampuni yanayofanya shughuli katika tasnia mbalimbali za kiteknolojia ili waweze kutumia ujuzi wao kuibadilisha Tanzania na dunia kwa ujumla,” alisema.

 

Smart Lab ni jukwaa la uvumbuzi linalounganisha wanafunzi wa vyuo vikuu pamoja na viongozi wa kampuni mbalimbali za kiteknolojia kwa lengo la kuwajengea uwezo wanafunzi hao kutumia vipaji hivyo kutatua changamoto mbalimbali kwa jamii.

NA MWANDISHI WETU

Leave a Comment