Katika kuunga mkono jitihada za serikali za kuboresha elimu nchini, Kampuni ya Uhandisi wa Umeme na Mitambo viwandani na Migodini ya Magare Ltd, imemuomba Mkuu wa shule ya sekondari ya Isagehe iliyopo katika halmashauri ya mji wa Kahama, mkoani Shinyanga, kuajiri walimu sita wa ziada wa masomo ya sayansi na biashara.
Walimu hao watakuwa wanalipwa mishahara na kampuni hiyo ili kuongeza ufaulu kwa wanafunzi wanaohitimu kidato cha nne.
Mkurugezi Mtendaji wa kampuni hiyo, Bw Mabula Magangila ametoa ahadi hiyo kwenye mahafali ya 20 ya kidato cha nne ya shule ya sekondari ya serikali ya Isagehe ambapo pamoja na kuwalipa mishahara walimu hao ameahidi kukamilisha maboma ya madarasa matatu ambayo ujenzi wake unasuasua.
Awali mkuu wa shule hiyo, Adolf Kabyemela, katika risala yake alisema shule hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo upungufu wa walimu wa masomo ya biashara na sayansi, madarasa pamoja na kompyuta.
Baadhi ya wanafunzi wa kidato cha nne wameahidi kufanya vizuri katika mtihani wa taifa licha ya mwaka huu kukumbana na changamoto ya mlipuko wa virusi vya Corona.
Na Mwandishi wetu
