
MKURUGENZIUwekezaji wa GSM, Injinia Hersi Said ni kama amewatisha wapinzani wao Simba baada ya kutoa kauli kuwa baada ya kufanikisha usajili wa beki wa Coastal Union, Bakari Mwamnyeto, sasa unafuata usajili wa kishindo na kihistoria wa wachezaji wa kigeni.
Hiyo ikiwa ni siku chache tangu wakamilishe usajili wa Mwamnyeto aliyekuwepo kwenye mipango ya kusajiliwa na Simba kabla ya Yanga kumuwahi na kumpa mkataba wa miaka miwili ya kuichezea timu hiyo kwa dau la Sh 150m.
Usajili mwingine wa kishindo ambao wameufanya Yanga ni wa mshambuliaji wa Mbao FC, Waziri Junior ambaye ilidaiwa pia alikuwa akiwaniwa na Simba pamoja na Azam, ambapo Yanga walimpata baada ya kumficha kwenye hoteli kubwa jijini Mwanza muda mfupi baada ya kumalizika mechi ya mwisho ya Mbao wiki iliyopita.
Akizungumza na Championi Ijumaa, Hersi alisema kabla ya usajili kufungiliwa aliahidi kufanya usajili mkubwa na wa kishindo.

Alisema kuwa sasa nguvu zao wamezielekeza kwenye usajili wa kimataifa kwa kuhakikisha wanafanya usajili wa kishindo na kuwashtua watani wao wa jadi, Simba waliokuwepo kwenye vita kubwa ya usajili katika msimu ujao.
“Kama unakumbuka vizuri kabla ya usajili mkubwa kufunguliwa nilitoa ahadi ya kufanya usajili wa kishindo na kushtua ambao tayari tumeufanikisha kwa kumsajili Mwamnyeto tuliyekuwa tunamgombea na watani zetu Simba.
“Hivyo baada ya hapo ninaahidi kuwapa sapraizi mashabiki wa Yanga kwa kufanya usajili mkubwa wa kishindo wa mchezaji kutoka nje ya nchi, ninafahamu mashabiki wana hofu kubwa baada ya kuachana na baadhi ya wachezaji.
“Tunachosubiria ni anga za nchi ambazo wachezaji wetu wanatokea ifunguliwe baada ya hapo ndiyo nyota wetu hao wataanza kutua nchini tayari kwa ajili ya kusaini na kujiunga na kambi ya pamoja iliyopangwa kuanza Agosti 10, mwaka huu,” alisema Hersi.
Stori: Wilbert Molandi, Dar es Salaam