TFF imesema imepokea kwa masikitiko madai ya Mwenyekiti wa Yanga SC, Dkt. Mshindo Msolla aliyedai kupitia Vyombo vya Habari kuwa Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji haijasikiliza shauri la klabu hiyo dhidi ya Simba SC.
TFF imemwandikia barua Dk. Msolla ikimtaka kujieleza kuhusu shutuma alizotoa dhidi ya Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji.
“Yanga iliwasilisha shauri mbele ya Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ikidai kuwa Simba ilikuwa inamshawishi mchezaji wao Bernard Morrison ajiunge na klabu yao akiwa na akiwa bado ana mkataba nao.
“Wakati Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ktk kikao chake cha July 2, 2020 ikianza kusikiliza shauri hilo, Yanga kupitia kwa Kaimu Katibu Mkuu, Wakili Simon Patrick aliomba kuliondoa kwa maelezo kilichowasilishwa ilikuwa taarifa tu kwa Sekretarieti ya TFF sio shauri.
“Kutokana na maelezo hayo ya Mlalamikaji (Yanga) Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ililiondoa shauri hilo. “Hivyo, madai ya Mwenyekiti wa Yanga, Dkt. Mshindo Msolla kuwa Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji haijasikiliza shauri hilo si ya kweli. Lengo lake ni kutaka kuichafua TFF.” imesema Taarifa hiyo.

