×

Johari Bado Hajampata Mtu Sahihi Maishani!

BLANDINA Chagula ‘Johari’ si jina geni kabisa kwa wapenzi wa filamu na wadau wa sanaa Bongo kutokana na kujihusisha na sanaa hiyo tangu kitambo, enzi za Kaole Sanaa Group ambapo huko ndipo alipopatia umaarufu wake.

 

Msanii huyu ambaye yuko kwenye tasnia hiyo kwa zaidi ya miaka 20 sasa, amesema kuwa hana papara ya kuolewa, kama bado hajampata wake ambaye ataweza kumnadi na kumuonesha kwa watu na kwenye mitandao lakini Mungu akimpatia atafanya hivyo.

 

Amani limezungumza nayo mambo mbalimbali kama ifuatavyo:

Amani: Vipi Johari mbona umepoa sana, mpaka sasa wameibuka watu wengine wameweza kufunika jina lako kabisa unafikiri ni kwa nini?

 

Johari: Unajua siku zote avumae baharini ni papa, kumbe wengine wapo, mimi sibabaishwi na waliokuja hivi sasa, kwa sababu natambua vizuri kabisa jinsi ninavyofanya kazi, kwa maana mimi ni mtunzi, muongozaji, mara nyingi kwa sasa nakaa nyuma ya kamera tu.

 

Amani: Lakini sasa hivi naona kama soko la filamu limeporomoka, ingawa bado naona unaendelea kukomaa, unawezaje kuidhibiti hali hiyo?

Johari: Unajua kila kitu siku zote ni kujipanga tu, na kuhakikisha kitu unachokitoa ni bora hata kikienda kwa mtazamaji anakikubali kweli ni kazi nzuri.

 

Amani: Kipindi cha nyuma Johari ulikuwa ni nadra sana kuonekana kujumuika na wenzako kwenye ishu mbalimbali za sanaa lakini sasa hivi nakuona ni mstari wa mbele nini kimekuhamasisha?

Johari: Nafikiri kila jambo na wakati wake, zamani kulikuwa na kazi nyingi sana za kutengeneza filamu na tulikuwa hatuwezi kutoka wote tukaacha ofisi wazi.

 

Amani: Mastaa wengi wamekuwa wakiweka wazi mahusiano yao ya kimapenzi wazi. Vipi kwa upande wako, mbona unayaficha?

Johari: (Kicheko) siyo kama nayaficha, lakini bado sijampata mtu sahihi wa kumnadi kwa watu, maana nitakuwa naonyesha mtu kesho tumemwagana, halafu na mimi nikaingizwa kwenye listi ya wasanii wenye msululu wa wanaume.

 

Amani: Kwa hiyo mpaka sasa huna mpenzi?

Johari: Na ndiyo maana kila siku namuomba Mungu, anipe na mimi wa kwangu najua atajibu tu maombi yangu.

Amani: Vipi kuhusu kupata mtoto, maana mastaa wengi sana hawajaolewa lakini tayari sasa hivi wana watoto, wewe umejipangaje kwa hilo?

 

Johari: Mbona mimi nina mtoto, kwani hamjui?

Amani: Mbona hujawahi kumuweka kwenye mitandao kama wanavyofanya wengine na umezaa na nani?

Johari: Mtu niliyezaa naye ndiyo siwezi kumuweka wazi, na kuhusu mtoto mbona namuwekaga tu.

 

Amani: Kumekuwa na madai siku hizi umekuwa mtu wa kilevi sana mpaka umepitiliza, vipi kuhusu hilo?

Johari: Sidhani kama kuna ukweli kuhusu hilo kabisa, kwa sababu hakuna mtu anayemzuia mtu kufanya kitu akipendacho.

Amani: Una kitu kingine unatarajia kufanya zaidi ya filamu?

 

Johari: Ndiyo, kuna biashara najipanga nataka kufanya kama ikikamilika, nitaiweka wazi tu.

Amani: Huko nyuma ilidaiwa mlikuwa kwenye bifu kali sana na Chuchu Hans, lakini sasa hivi naona ni marafiki na mnafanya kazi pamoja nani aliwashauri hilo?

 

Johari: Hakuna aliyetushauri, tuliona hayo mambo ni kama ya kitoto, tukaamua kufanya kazi kuliko kukalia majungu, maana na watu ndiyo walikuwa wakituchochea zaidi.

Amani: Vipi kuhusu Ray, maana ndiyo kilidaiwa ndicho chanzo cha wewe na Chuchu, kugombana kila wakati, unazungumziaje hilo?

 

Johari: Hapana jamani, hayo mambo ya kitambo sana na yalishapitwa na wakati, sasa hivi kila mtu ana mambo yake na maisha yake na tulishasahau hiyo habari kabisa, tunapiga kazi.

Amani: Johari umekuwa hauwezi kucheza filamu ya mtu yeyote kwa sasa na umeonekana kwenye filamu chache sana, kwa nini?

 

Johari: Hiyo ilikuwa ni zamani jamani, sasa hivi naweza kucheza filamu mbalimbali mpaka tamthiliya, sasa hivi sichagui chochote.

Amani: Umekuwa kwenye tasnia kwa muda mrefu sana, nini ambacho umefaidika nacho?

 

Johari: Hakuna jipya, mambo ni yaleyale ya kupata umaarufu, pasipo kitu chochote zaidi ukipita sehemu unavutwa shati, huwezi kula kwa mama ntilie, na huwezi kupanda daladala basi.

Amani: Asante sana Johari, nashukuru sana kwa ushirikiano wako.

Johari: Karibu sana!

MAKALA: IMELDA MTEMA

Leave a Comment