SERIKALI imesema haijazuia maudhui ya redio za nje kusikika nchini bali imeagiza maudhui hayo yapate kibali kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ili kulinda na kuheshimu maadili ya nchi.
Waziri wa Habari, Dkt. Harrison Mwakyembe amesema, “Serikali haijakataza redio za ndani kujiunga au kupokea maudhui kutoka redio na chaneli za nje bali kinachotakiwa kufanyika ni kufuata utaratibu ambao Serikali imeweka.”
Ameongeza kwamba sekta ya habari imesimamiwa na Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016. Amewataka wanahabari kufanya kazi kwa kuzingatia sheria hiyo inayoeleza kwa kina suala la weledi katika taaluma, ukweli na uwazi katika kuchakata habari.
Amewataka waandishi wa habari katika kipindi hiki cha uchaguzi mkuu, lazima watumie kalamu zao vizuri kwa kuandika na kutangaza habari zenye ukweli, uwazi na ambazo hazionyeshi upendeleo wowote kama ambavyo taaluma ya habari inataka.
