NAIBU Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, amefunguka na kutolea ufafanuzi kuhusu miradi mbalimbali ya maji ambayo inatekelezwa na serikali ya awamu ya tano kuondoa kero ya maji nchini pamoja na changamoto zinazojitokeza kwenye sekta ya maji nchini.
Hayo ameyasema leo Alhamisi, Agosti 13, 2020 asubuhi wakati akifanya mazungumzo na Front Page ya +255 Global Radio.
“Mpaka sasa tumetekeleza miradi 2,556, tangu Rais Magufuli aingie madarakani miradi iliyokamilika ni 1,423, upatikanaji wa maji umeongezeka kutoka asilimia 47 hadi 70 kwa vijijini, mijini ni kutoka asilimia 74 hadi 85, mpaka Desemba miradi 200 itakuwa imekamilika.
“Pale Mwandiga tuna mradi mkubwa tuliotekeleza kwa ajili ya Manispaa ya Kigoma, tukasema maji hayawezi kuwa Kigoma halafu Mwandiga yakosekane, tumetumia mabilioni ya pesa, ndiyo maana nikawapa siku 14 wafunge pampu na watu wa Mwandiga wapate maji.
“Kila mwananchi ana haki ya kupewa huduma ya maji, naye ana wajibu wa kulipia huduma ya maji. Inatakiwa msoma mita amshirikishe mtumiaji wa huduma za maji wakati wa kusoma mita, aone na asaini kwamba mwezi huu ametumia unit 20.
“Pale Shinyanga Vijijini tulikuwa na mradi, pesa zote zimelipwa, mradi umekamilika lakini maji hayatoki, nikamuuliza mkandarasi akasema sijawahi kuona wananchi wachawi kijiji hiki, mabomba yanapaa kama Bombardier usiku, nikasema wewe mjinga kabisa,” Jumaa Aweso.
