UONGOZI wa umetamba kuwa kuondoka kwa kiungo wao mshambuliaji raia wa Ghana, Bernard Morrison hakuwapi presha yoyote badala ya kufanikisha usajili wa Farid Mussa.
Yanga imefanikisha usajili huo juzi baada ya kumtangaza nyota huyo aliyesaini mkataba wa mwaka mmoja wa kukipiga Jangwani akitokea Klabu ya Tenerife ya nchini Hispania.
Farid anakamilisha idadi ya wachezaji saba wapya waliosajiliwa Yanga katika kuelekea msimu ujao wengine ni Yassin Mustapha, Zawadi Mauya, Kibwana Shomari, Bakari Mwamnyeto, Waziri Junior na Abdallah Shaibu ‘Ninja’.
Akizungumza na Championi Jumamosi,Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Yanga, Hassan Bumbuli alisema kuwa, usajili huo wa Farid umetokana na mahitaji ya benchi la ufundi baada ya kuhitaji winga mwenye uwezo mkubwa wa kufunga, kutengeneza mabao kwa njia ya kupiga krosi.
Bumbuli alisema kuwa hawajutii usajili huo wa Farid walioufanya ambao kutokana na sifa ambazo nyota huyo mwenye kasi akiwa anakokota mpira kushambulia goli la wapinzani wao.
Aliongeza kuwa baada ya kukamilisha usajili wa wachezaji wa ndani, hivi sasa nguvu zao wamezielekeza kwa wachezaji kutoka nje ya nchi ambao wataanza kutua kuanzia leo Jumamosi baada ya anga za nchi ambazo wachezaji hao kufunguliwa baada ya kufungwa kwa muda kutokana na janga la Corona.
“Tunaamini Farid ni chaguo sahihi kwa sasa ndani ya timu ya wananchi na tunafurahi kukamilisha usajili wake ambao unaonekana una manufaa makubwa kwetu.
“Usajili huu wa Farid ndiyo tuliokuwa tunauhitaji, kwani benchi la ufundi lilitoa mapendekezo ya kumsajili kiungo wa kutokea pembeni mwenye ubora atakayefunga na kutengeneza mabao kwa kutumia krosi.“Farid ni kati ya viungo wa pembeni bora wenye uwezo, uzoefu mkubwa wa kucheza ligi ya ndani na michuano ya kimataifa, mashabiki wampe ushirikiano,” alisema Bumbuli.
Stori: Wilbert Molandi na Careen Oscar

