Baada ya mwanamuziki mkubwa barani Afrika, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ kutangaza kufunga ndoa Oktoba 2, mwaka huu, kitendawili kikubwa kimekuwa ni nani anayeolewa?
Hata hivyo, Gazeti la IJUMAA limenasa ubuyu wa motomoto (exclusive) kutoka kwenye baadhi ya vyombo vya habari katika nchi jirani ya Rwanda, ambavyo vimemuibua mrembo mmoja vikimtaja kuwa ndiye mchumba anayeolewa na Diamond au Mondi.
NI ZAMU YA RWANDA
Kwa mujibu wa mitandao ya habari za burudani nchini Rwanda, Mondi amepania kumaliza Afrika ya Mashariki baada ya kutua kwa mrembo huyo ambaye ni mtoto wa tajiri mkubwa nchini Rwanda, ambaye sasa anakwenda kutulia naye.
UGANDA TAYARI
Kabla ya kutua kwa mrembo huyo ambaye alikutana naye kwa mara ya kwanza jijini Kigali, Rwanda, miaka minne iliyopita alipokwenda kwa ajili ya shoo, tayari amepita na mwanamama kutoka Uganda na kuzaa naye watoto wawili, Tiffah na Nillan; Zarihan Hassan ‘Zari The Boss Lady’.
TANZANIA TAYARI
Kutoka Tanzania, Mondi amezaa mtoto wa kiume aitwaye Dyllan na mwanamitindo Hamisa Mobeto.
KENYA TAYARI
Kwa upande wa Kenya, pia Mondi amezaa mtoto mmoja wa kiume aitwaye Naseeb Junior na msanii wa muziki wa Kizazi Kipya, Tanasha Donna.
NCHI ZILIZOBAKI
Imeelezwa kuwa, baada ya kuifikia Rwanda, sasa zitakuwa zimebaki nchi mbili tu za Afrika Mashariki ambazo hazijafikiwa na Mondi, ambazo ni Burundi na Sudani Kusini ili kufikisha idadi ya nchi sita zinazounda Jumuiya ya Afrika Mashariki.
TURUDI RWANDA
Mitandao ya Rwanda imethibitisha pasi na shaka kwamba, Mondi ambaye ni Rais wa Lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB), sasa ni rasmi anakwenda kutia nanga nchini humo.
Imeelezwa na mtandao mmoja kuwa, Mondi ni mjanja kutoka Kitongoji cha Tandale jijini Dar ambaye amepata ‘Miss Right’ (mrembo sahihi kwake kutoka nchini Rwanda).
Akiwa jijini Dodoma wiki mbili zilizopita, Mondi aliwaambia mashabiki wake kuwa, tayari amemchumbia mwanamke mmoja ambaye amepanga kumuoa Oktoba 2, mwaka huu atakapokuwa akisherehekea siku yake ya kuzaliwa ambapo atakuwa anatimiza umri wa miaka 31.
Kabla ya kutua kwa mrembo huyo wa Rwanda, Mondi alimchumbia Tanasha, lakini waliishia kupata mtoto bila kufunga ndoa kama ilivyokuwa kwa Zari ambapo waliishia kuahidiwa tu bila utekelezaji.
Imeelezwa kuwa, jambo ambalo wengi hawalijui ni kwamba, tayari Mondi; ndugu, jamaa na marafiki wa ndani wamekuwa wakipanga taratibu mbalimbali za kwenda kulipa mahari ya nguvu kabla ya kufungwa kwa ndoa. Inasemekana kumekuwa na vikao vya hapa na pale kwa ajili ya kupanga siku ya kupeleka mahari ya kueleweka kwa mrembo huyo Mnyarwanda aliyekwenda hewani mithili ya twiga.
MAKONDA NDA NI…
Kwa mujibu wa mitandao hiyo, kiungo mchezeshaji wa tukio hilo ni aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ambaye amebebeshwa jukumu zito la kuhakikisha shughuli hiyo inakamilika kwa kiwango cha juu kabisa.
HELLEN KAZIMOTO…
Kiungo mwingine muhimu anayetajwa kwenye zoezi hilo ni Meneja wa Matukio na Maisha ya Wanamuziki wa Wasafi, Hellen Kazimoto.
NDOA YA SIRI
Pia mitandao hiyo imeeleza kuwa, zoezi hilo litatanguliwa na ndoa ya siri ya Kiislam ambayo itafungwa ndani ya mwezi huu (Agosti) au Septemba, kisha itafuata ile sherehe ya kukata na shoka ya Oktoba 2, mwaka huu ambayo awali inaweza kufanyika jijini Kigali, Rwanda kabla ya kurejewa jijini Dar es Salaam, Tanzania.
“Huyu mrembo ni Muislam, kwa hiyo Agosti au Septemba, kutakuwa na ndoa ya kimyakimya ya Kiislam, itahusisha wanafamilia na marafiki wa karibu pekee, lakini shughuli ya wote ni Oktoba 2,” ilisomeka sehemu ya habari hiyo kubwa kwenye mitandao hiyo ya Rwanda.
MREMBO HUYU NI NANI?
Gazeti la IJUMAA limechimba kwenye vyanzo vyake na kutajiwa jina lake kuwa anaitwa Shaddy Boo.
Shaddy Boo ni mrembo maarufu kwenye mitandao ya kijamii (sosholaiti) ambaye mwaka 2016 alidai kunaswa hoteli moja jijini Dar akiwa na Mondi ambapo miongoni mwa mambo yaliyozua gumzo ni kitendo cha mrembo huyo kuonekana amevaa viatu vya wazi ambavyo vilivaliwa na Mondi wakati anaingia hotelini hapo.
Hata hivyo, wakati mrembo huyo akiondoka Tanzania, alinaswa na vyombo vya habari kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar na alipoulizwa juu ya uhusiano wake na Mondi, alijibu;
“Nothing much is going on, we are just friends yeah!
Aah! No!, it’s not true, we are just friends. (Hakuna cha zaidi kinachoendelea, sisi ni marafiki wa kawaida tu yeah! Aah! Hapana! Si kweli, sisi ni marafiki wa kawaida tu)”
TUJIKUMBUSHE
Si mara ya kwanza kwa mrembo huyo kuhusishwa na Mondi, kwani mwezi Septemba, 2018 alitua Bongo ambapo alikuwa hosti wa Shoo ya Jibebe Challenge iliyoandaliwa na Mondi kupitia wimbo wake wa Jibebe na kampuni moja ya kubeti.
Siku chache baadaye, zilisambaa picha zake kwenye mitandao ya kijamii akiwa kitandani amejifunga taulo jeupe.
Hata hivyo, mazingira ya chumba na kitanda, yalikuwa hayana tofauti na picha za Mondi zilizomuonesha naye akiwa kwenye chumba, kitanda na taulo hilohilo, huku akiwa kifua wazi.

