KATIKA hali isiyo ya kawaida, jana watu wanaodaiwa kuwa ni polisi walitinga kwenye mazoezi ya Simba na kuingia moja kwa moja uwanjani kitendo ambacho kilimkasirisha kocha mkuu wa timu hiyo, Mbelgiji, Sven Vandenbroeck ambaye alichukua uamuzi wa kuwatimua.
Kikosi cha Simba, jana Jumatano kiliendelea na mazoezi yake ya kujiandaa na msimu wa 2020/21 kwenye Uwanja wa Simba Mo Arena, Bunju jijini Dar es Salaam.
Wakati nyota wa Simba wakifika uwanjani hapo kwa ajili ya mazoezi, aliyekuwa Mtendaji Mkuu wa Simba, Crescentius Magori, alitinga mazoezini hapo na gari lake, huku nyuma kukiwa na gari ambalo linadaiwa lilibeba polisi waliokuwa wamevaa nguo za kiraia.
Magori alipoingia uwanjani hapo, watu hao nao waliingia uwanjani, kitendo ambacho Sven alihoji na kutaka kuwafahamu kwani hawana ruhusa ya kuingia eneo ambalo yeye ndiye bosi.
Spoti Xtra lilishuhudia tukio hilo, ambapo baada ya mvutano wa muda mrefu, watu hao waliamua kuondoka na kumuacha Sven akiendelea na program zake.
Wakati huohuo, Kiungo wa Simba, Francis Kahata, jana alifanya mazoezi na wenzake baada ya kurejea nchini akitokea mapumzikoni nyumbani kwao Kenya.
STORI: JOEL THOMAS NA CAREEN OSCAR, DAR

