MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Dkt. John Magufuli amewahakikishia wajumbe wa Mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC) kuwa amepitia majina ya watia nia wanaowania kuteuliwa kugombea ubunge kupitia chama hicho, ambapo kazi kubwa imefanyika ili kuakikisha chama kinapata watu sahihi watakaoweza kuleta ushindi katika uchaguzi mkuu ujao.
Magufuli amesema hayo leo Alhamisi, Agosti 20, 2020 wakati akifungua mkutano huo katika Makao Makuu ya CCM, Dodoma na kueleza kwamba makabrasha yote wameyapitia na kutenda haki kwa wanaostahili wala hajaonewa mtu.
“Niwapongeze wajumbe wote wa NEC kwa kunipigia kura nyingi za NDIYO, mlikuwa wajumbe hamkuniangusha wajumbe, hata kwenye udhamini mmenipa wadhamini zaidi ya milioni 1.1. Nimedhaminiwa katika mikoa mingi sana ya Bara na Zanzibar.
“Nawapongeza sana wana-CCM wote walioomba kuteuliwa kuwania nyadhifa mbalimbali, ubunge 10,367, uwakilishi 786, udiwani 33,094, hii inaonyesha CCM inapendwa sana, hakuna chama kingine ambacho watu wengi namna hii wamejitokeza, CCM ni chama kinachoheshimika.
“Naomba niwahakikishie kuwa uchambuzi huu ulikuwa wa kina kwelikweli, tumetumia vyanzo vyetu vyote, nimepitia majina yote 10,367. Hatujampendelea mtu wala kumnyima mtu haki yake, tumewajadili wagombea wote kwa kina na kujiridhisha wenye sifa.
”Wabunge na Wawakilishi ndiyo wasemaji wa wananchi hivyo ilikuwa lazima tujiridhishe kuwa tutakapowapitisha wawe na uwezo wa kuyafanya hayo na mengine kwa uwezo mkubwa.
“Sisi tumefanya kazi kubwa kwa siku mbili ya kuchambua kwa kina ili kuwarahisishia ninyi kazi ya leo. Niwaombe wajumbe wote wa Halmashauri Kuu Taifa tujadili majina ya wagombea bila kujali undugu wala ukanda, tumtangulize Mungu mbele,” amesema Magufuli.
Awali, Dkt. Bashiru Ally, ambaye ni Katibu Mkuu wa CCM amesema; “Kutokana na ratiba ya uchaguzi ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kikao hiki hakitapitisha majina ya wagombea uwakilishi, kitapitisha majina ya wagombea Ubunge wa Majimbo na Wagombea Ubunge wa Viti Maalum.”
