MWENYEKITI wa Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), Hashim Spunda Rungwe ameendelea kukazia kuwa sera ya Chama chake katika uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu ni kuhakikisha wanafunzi mashuleni wanapata chakula ili wawe na afya na waweze kusoma vizuri kutengeneza taifa la kesho.
Rungwe ambaye ni mgombea Urais kupitia chama hicho, amesema hayo leo Alhamisi, Agosti 20, 2020 wakati akifanya mahojiano na +255 Global Radio kupitia Kipindi cha Front Page.
“Nilichojifunza kwenye siasa ni kwamba wananchi ndiyo wanaamua nani awe kiongozi wao, na wakipewa fursa wanaamua kweli.
“Nikichaguliwa nitahakikisha kila mtoto anapata chakula shuleni na chakula ndiyo kitakuwa msingi wa Taifa hili, lazima mtoto ale ndipo asome vinginevyo atakuwa zezeta tu, sera yetu ni chakula, elimu na maendeleo.
“Sisi vyama vya siasa tuna madhaifu yetu lakini niseme tu kwamba, kwenye uchaguzi huu Muungano utakuwepo, iwe kwa hadhara au kwa siri, si lazima mpaka mtengeneze jina la Muungano na kuli-brand.
“Mimi ndiyo nafaa kuuwakilisha upinzani kwenye kinyang’anyiro cha urais 2020 na si mwingine, hii haihitaji umaarufu, kwanza mimi ninakaa na wananchi mtaani kila siku, nashiriki nao mambo mbalimbali, ninaamini wananikubali.
