ILIPOISHIA
“Lakini sisi tuna bunduki, tunaweza kukabiliana na hatari yoyote.”
“Huyo jini kama tutamkuta, sidhani kama bunduki yenu inaweza kusaidia.”
“Kwani wewe ulimuona huyo jini kwa macho yako?”
SASA ENDELEA..
“Nilimuona mara kadhaa, yuko kama binadamu.”
“Na ulimuona akiwafyonza damu hao watu na kuwala ubongo kama ulivyotueleza?”
“Nilimuona. Hata yule mtu niliyewaonesha pale niliona wakati akifyonzwa damu.”
“Sasa huyo msichana anayeishi na huyo jini anaishi naye vipi?’
“Anaishi naye kama mke wake. Alimleta katika hili pango kimiujiza. Huko kwao hadi leo hawajui yuko wapi.”
“Umetueleza mkasa wa ajabu lakini tukimpata huyo msichana tutakuwa na hadithi nzuri sana.”
Kwa bahati njema hatukusumbuka sana tukafika katika ule mlango wa kuingilia mahali alipokuwa anaishi Faiza.
“Nafikiri ni hapa,” nikawaambia.
Wale watu wakatazamana kwa mshangao. Kitu cha kwanza kilichofanya waamini maneno yangu, bila shaka ni ile harufu iliyokuwa ikisikika mahali pale. Ilikuwa harufu tofauti na iliyokuwa ikisikika sehemu nyingine tulizopita.
Pale palikuwa na harufu ya jasho la kibinadamu pamoja na harufu ya vyakula.
Yule mtu aliyeshika bunduki alinitolea macho ya taharuki akaniambia.
“Sasa ingia twende ukatuoneshe huyo msichana.”
“Wewe mwenye bunduki ndiyo ungetangulia,” nikamwambia.
“Sasa mimi nitajua tunakwenda upande gani?”
“Nitakuwa nyuma yako nitakuelekeza.”
Yule mtu akakubali kutangulia, mimi nikawa nyuma yake. Yule mwenzake akabaki nyuma yetu.
“Yuko wapi? Yuko wapi?” Ilikuwa sauti ya yule mtu aliyeshika bunduki. Aliuliza hivyo huku akiangalia kila upande.
“Twende tu,” nikamwambia.
Watu hao wakaanza kuona mazingira tofauti na kule tulikopita. Waliona ukumbi kama sebule. Wakaona mapazia yaliyokuwa yamewekwa katika sehemu za kupitia.
Yule aliyetangulia kila mara alikuwa akitazama nyuma kama vile alikuwa anataka kuhakikisha kama bado tupo nyuma yake. Bila shaka alikuwa ameshapata uoga.
Niliwaongoza hadi katika sehemu aliyokuwa anakaa Faiza. Tukapenua pazia na kuingia.
Faiza alikuwa amelala lakini tulipoingia tu akaamka.
“Ni kina nani nyinyi?” Akatuuliza.
Nikajitokeza mbele yake.
“Ni wewe? Umekuja na kina nani?” Akaniuliza.
“Ni watu walioingia katika hili pango kututafuta. Wametaka niwalete kwako wakuone.”
Faiza akainuka na kusimama. Akawa anawatazama wale watu.
“Jamani Faiza mwenyewe ndiye huyu,” nikawaambia wenzangu.
“Sasa tumeamini. Wewe umekuwa ukiishi ndani ya pango hili siku zote hizi?” yule aliyekuwa na simu akamuuliza.
“Ndiyo, nimekuwa nikiishi hapa,” Faiza akamjibu”
“Unaishi na nani.?”
“Ninaishi na jini.”
“Jini ndiye aliyekuleta hapa?”
“Ndiyo.”
“Kwenu ni wapi?”
“Bagamoyo, mkoani Pwani.”
“Umeishi humu kwa muda gani?”
“Miaka minne.”
“Huyo jini yuko wapi?”
“Ameshaondoka.”
“Sasa tunataka uondoke na sisi, uko tayari?”
“Niko tayari lakini huyo jini akitokea patawaka moto!”
“Huwezi kuendelea kuishi humu, kwa vyovyote vile ni lazima tukutoe.”
Hapo hapo milio ya ajabu ajabu ikaanza kusikika kutoka katika ile chupa ya Kaikush. Nilipoitazama niliona moshi unajaa. Nikajua Kaikush anakuja.
Faiza akatutahadharisha.
“Jamani mwenye sehemu hii anakuja!”
“Ni nani?” aliyeshika bunduki akauliza kwa taharuki.
“Ni huyo jini niliyewaambia, huyu mwenzenu anamfahamu. Anaua watu wote wanaofika hapa.”
“Umesema anakuja, yuko wapi sasa?” mwenye bunduki aliendelea kuuliza huku akitazama kila upande. Bunduki yake alishaiweka sawa mikononi.
“Anatokea kwenye ile chupa inayojaa moshi. Hiyo milio mnayoisikia ni yake. Punde tu mtamuona. Mimi nakimbia.” nikawambia.
“Unakimbia nini. Acha aje hapa tumuone. Tuko wanaume watatu na tuna bunduki, tunaogopa nini?”
“Tulikuwa wanaume sita na wenzangu wote wameuawa, itakuwa sisi watatu,” nikajiambia kimoyomoyo.
ITAENDELEA