The House of Social Media
gunners X

Nelly muosha magari wa Posta -12

0

ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA:

Mpenzi msomaji, wiki iliyopita niliishia pale Nelly alipomwambia yule mrembo kwamba alikuwa na hela za kununulia simu ya kisasa hivyo dada huyo kubaini kwamba, Nelly alikuwa na kiasi kisichopungua shilingi laki mbili, akaamua kumpa namba zake kwa lengo la kumpiga mizinga mpaka akome. SONGA MBELE…

“Sasa hiyo namba utaindika wapi?” yule mrembo akamuuliza Nelly.
Nelly alicheka na kumwambia amtajie ataikariri, ndipo mrembo akamuuliza kama kweli anaweza kuikariri, Nelly akamwambia amtajie tu wala asihofu angeiweka kichwani.

Baada ya yule msichana kumtajia Nelly alimwambia alishaidaka na asingeisahau, mrembo alipomwambia amtajie Nelly akaitaja bila kukosea, mrembo akaishia kumpongeza kwa kuwa na kichwa chepesi.

Safari iliendelea ndipo fundi Yassin alibaini huko mbele ya safari dogo ambaye hakuwa na fedha kabisa angeumbuka, akageuka na kumwambia Nelly kwamba akifika Tandika atakwenda kumuona yule Mwarabu aliyemletea simu yake.
Nelly alijua nini kilikuwa kikiendelea baina yake na fundi wake, akamwambia sawa ndipo fundi akafungua pochi yake akachomoa wekundu watatu wa msimbazi na kumwambia aweke mfukoni.

Nelly alichukua fedha hizo akiwa anatabasamu na kuzisunda mfukoni huku akimsifia sana fundi wake kwa kujiongeza, basi lilipofika kwenye Mataa ya Veta, yule mrembo alimwambia Nelly kwamba, anasogea mbele kwani alikaribia kufika.

Baada ya kusema hivyo, sharobaro Nelly alimwambia asiwe na wasiwasi naye atashukia hapo kwani alikuwa akihitaji kwenda kumuona rafiki yake Mitaa ya Keko, Fundi Yassin alipomsikia Nelly akitoa kauli hiyo, akajisemea moyoni;
“Mrembo ameshaumia leo, sharobaro ana wekundu watatu mfukoni!”
Kweli gari lilipofika Kituo cha Keko Bora, Nelly alimuaga Fundi Yassin kwamba anakwenda kumuona jamaa yake watakutana nyumbani kisha wakateremka na yule mrembo.

Wakiwa wamesimama kituoni, Nelly alimuuliza yule mrembo kama alikuwa na haraka sana ya kwenda nyumbani, mrembo akamwambia siyo kivile kwa sababu dada yake alikuwa amesafiri.
“Yap! Habari kama hizi ndiyo napenda kuzisikia,” Nelly alijisemea moyoni.
“Kwa hiyo tunaweza kutafuta sehemu japo tupate kinywaji kisha kila mmoja aendelee na safari zake?” Nelly alimuuliza yule mrembo.

Kufuatia yule mrembo kumuona Nelly alikuwa yupo vizuri kifedha, alimwambia hakukuwa na ubaya ndipo kijana huyo ambaye alikuwa na usongo wa yale mambo yetu baada ya kumkosa Doreen akamwambia amfuate.
Wawili hao walivuka barabara na kuanza kurudi walikotokea kisha wakakata kulia na kuingia kibarabara cha mtaani ambapo hawakutembea umbali mrefu wakakuta baa, wakazama ndani.

Msichana huyo ambaye mpaka muda huo Nelly hakulifahamu jina lake, hakuelewa kama baa waliyoingia kwa nyuma ilikuwa na vyumba a.k.a machinjio, walipoketi tu mhudumu alifika na kuwauliza aliwahudumie nini!
Nelly aliagiza kilevi yule mrembo aliagiza soda, kabla mhudumu hajaondoka Nelly alimuuliza kama alikuwa hatumii kilevi, mrembo akamwambia huwa anatumia lakini kwa siku ile hakujisikia tu!
“Kufuatia kauli hiyo, Nelly alimwambia anapojisikia vizuri anakunywa kilevi gani akamtajia ndipo akamwambia mhudumu amletee kilevi hicho na kuachana na soda.

“Yaani besti mimi ninywe kilevi wewe unywe soda wapi na wapi? Wewe leo kunywa tani yako suala la fedha siyo tatizo,” Nelly alimwambia yule mrembo kisha akamwita mhudumu wa jikoni.
“Mimi niletee mchemsho wa kuku, wewe utapenda kula nini?” Nelly alimwagiza mhudumu na wakati huohuo akamuuliza mrembo wake alihitaji kula nini.

“Kama ulivyoagiza wewe,” mrembo akamwambia Nelly ambaye alifurahi sana kwani alijua jioni ile ya saa moja angemuua tembo kwa bua.“Mimi nafikiri ungeagiza tofauti na mimi ili kila mtu aonje chakula cha mwenzake, unaonaje?” Nelly alimuuliza yule mrembo.

“Oke, basi mimi niletee ulimi na ndizi mbili, ndimu na pilipili weka pembeni,” yule mrembo aliagiza.
Baada ya kutoa oda hiyo, Nelly alimwambia alifanya vizuri, wakaendelea kunywa pombe waliyoagiza na kuendelea na stori za hapa na pale ndipo mhudumu wa jikoni akaleta msosi.
Alipowanawisha wakaanza kula na kupiga stori huku moyoni Nelly akisema: “Wewe leo lazima nikugaragaze kwani mla vya watu na vyake huliwa.”

Nelly alikata kipande cha mnofu wa kuku na kutaka kumlisha yule mrembo ambaye alikwepesha mdomo na kumwambia ampe mkononi, kijana huyo akafanya hivyo.

“Lakini unajua umenikosesha raha, mimi nilitaka kukulisha wewe umekwepesha mdomo?” Nelly alimwambia.
“Sijapenda tu si unajua mambo hayo hufanyiana wapenzi na si kila mtu?” yule mrembo alimwambia Nelly bila kujua kama kauli yake ilimuumiza sana.
“Najua sana ila sioni kama kuna tatizo mimi kukulisha si namna ya kupoteza mawazo baada ya kazi,” Nelly alimwambia.

Wakati wawili hao wakizungumza, mhudumu wa vinywaji alifika na kuchunguza chupa zilizokuwa na kilevi na kubaini vilibaki kidogo akavimimina kwenye glasi na kumuuliza Nelly kama aongeze.
“Hicho ndicho kilichotuleta hapa, kuepusha usumbufu leta mbili kwa kila mmoja, zote ziwe za moto kama ulizoleta mwanzo,” Nelly alimwambia.

Leave A Reply