Tarime vijijini ni mojawapo ya majimbo manne yanayonogesha Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28 mwaka huu. Majimbo mengine ni Kawe, Mbeya Mjini na Arusha Mjini.
Utamu wa majimbo haya, unatokana na ushindani mkubwa uliopo baina ya chama tawala –CCM na vyama vya upinzani hususani Chadema.
Vivyo hivyo katika jimbo la Tarime Vijijini ambalo ni ngome ya Chadema, sasa linawakutanisha mafahari wawili waliokua zizi moja … yaani John Heche (Chadema) na Mwita Waitara (CCM).
Jimbo hilo ni ngome ya Chadema kwa sababu awali lilikuwa jimbo moja la Tarime kabla ya mwaka 2015 kugawanywa na kuwa Tarime Vijijini na Mjini, ambako kote Chadema ilichukua katika uchaguzi mkuu wa mwaka huo.
Awali jimbo la Tarime kuanzia 2005 hadi 2008, lilikuwa chini ya Chacha Wangwe aliyekuwa Makamu mwenyekiti wa Chadema, 2008 hadi 2010 liliendelea kuwa ngome ya Chadema kupitia Charles Mwera.
Lakini kulipotokea mvurugano ndani ya Chadema na Mwera kutimkia CUF, mgombea wa CCM 2010 Nyambari Nyangwine alilinyakua kirahisi na kumwangusha Mwera- CUF, na Mwita Waitara (Chadema) ambaye alikuwa mshindi wa pili kwa tofauti ya kura 730 pekee katika uchaguzi huo.
Katika uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, Heche alishinda Tarime vijijini huku Esther Matiko akishinda Tarime mjini akiwa ndiye mwanamke wa kwanza kuongoza jimbo hilo tangu liasisiwe kuwa jimbo la Tarime mwaka 1960.
Hata hivyo, macho na masikio ya Watanzania na wana Mara, ni katika jimbo la Tarime Vijijini kutokana na tambo pamoja na mbwembwe ambazo zimetolewa na pande zote, yaani Waitara na Heche.
MWITA WAITARA UIMARA
Waitara ni mwanasiasa mkomavu ambaye amepitia ‘rabsha’ za pande zote, kwa maana ya CCM na Chadema. Kwa sababu kuanzia mwaka 1998 hadi 2008, alikuwa kada wa CCM ambapo alikuwa Katibu wa UVCCM Wilaya ya Kinondoni na baadaye Tanga.
Akiwa Chadema mbali na kuwa mbunge wa Ukonga kuanzia 2015, pia alikuwa Ofisa wa Sera na Utafiti wa Chadema kuanzia 2008 vilevile Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kivule hadi mwaka 2014.
Waitara ni mzungumzaji mzuri, mwenye uwezo wa kujenga hoja lakini jazba inamwangusha. Kwa sababu baada ya kuingia Chadema 2008 na baadaye 2018 kurejea CCM, alionesha uwezo mzuri ndani na nje ya Bunge, ndiyo maana Rais John Magufuli alimteua mara moja kuwa Naibu Waziri Tamisemi alipohamia CCM.
UDHAIFU
Jazba ni mojawapo ya udhaifu katika uzungumzaji wake, kwani katika baadhi ya mahojiano aliyofanya kituo kimojawapo cha runinga, alipandwa na jazba kiasi cha kushindwa kujibu kwa ufasaha maswali ya mwandishi aliyekuwa akimhoji.
Kujenga makundi ya wagombea ndani ya CCM, ni mojawapo ya udhaifu unaotajwa kuweza kumwangusha. Udhaifu huo ulijitokeza pindi alipoanza kile kilichotafsiriwa kuwa ‘kampeni mapema’ katika jimbo hilo, jambo ambalo lililazimu CCM mkoa wa Mara kumuita na kumuonya.
Makundi hayo yanadaiwa kuibuka kutokana na ujio wake wa ghafla kutoka Ukonga na kuhamia Tarime vijijini anakopaita kuwa ni nyumbani. Katika kura za maoni ndani ya CCM, hakupishana pakubwa na watia nia wenzake kwa sababu Waitara alipata kura (291), Eliakim Maswi (128) na Nyerere Mwera (122).
Koo kusalitiana. Ndani ya jimbo la Tarime vijijini, kuna koo zipatazo nane ambazo ni Wairege, Wanyabasi, Wakira, Watimbaru, Wakenye, Walenchoka, Waanchari, Wanyamongo, nje ya vyama vya siasa; koo hizi hupiga kura kwa kuangalia mtu wa koo yao halafu chama hufuata.
Hata hivyo, inaelezwa kuwa, koo hizi zimekuwa na migogoro ya mara kwa mara iliyofanya wasiaminiane. Licha ya kwamba ni faida kwa Waitara anayetokea koo ya Wairege, inaelezwa kuwa wanaweza kusalitiana kwa sababu Bwire naye ametokea katika koo hiyo.
Lakini usaliti ndiyo ‘dhambi’ inayomtesa kiongozi huyo machachari, usaliti huo unatokana na maamuzi yake ya kuhama kutoka CCM kuelekea Chadema na baadaye Chadema kurejea CCM. Kwamba wachambuzi wa siasa wanamuona kama mtu wa kutangatanga hata kama anatumia fursa hiyo kikatiba.
Hata hivyo, kitendo cha kulikacha jimbo la Ukonga ambalo lilimwandikia historia ya kuwa mbunge na kurejea Tarime ambako anaita ni nyumbani bila kuwa na kumbukumbu kuwa ndiko alikoangushwa mwaka 2010, ni mojawapo ya ajenda inayotajwa kuwa ni sawa na usaliti kwa wapiga kura wa Ukonga.
JOHN HECHE UIMARA
Kama ilivyo kwa Waitara, Heche ni mzungumzaji mzuri anayeweza kulimiki jukwaa, anaweza kujenga hoja kuitetea na kushawishi wananchi au wasikilizaji kumuelewa na kumuunga mkono.
Kipaji hiki ndicho kilichomvuta kutoka Chuo kikuu cha St Agustine alipokuwa akisoma mwaka wa pili na kuja kugombea ubunge ndani ya Chadema kwa mara ya kwanza mwaka 2010 kabla ya kukosa kura na kuamua kugombea udiwani nafasi ambayo aliipata na kuitumikia hadi 2015.
Licha ya kwamba yapo maeneo anayotajwa kutotekeleza ahadi zake, lakini kama mbunge, yapo mambo aliyoyafanya, hivyo kumjengea uaminifu kwa wapiga kura wake.
Hata hivyo, mgawanyiko ndani ya CCM unatajwa kuweza kumbeba Heche, hasa ikizingatiwa tayari amejenga ngome ya Chadema ndani ya jimbo hilo katika kipindi cha miaka mitano aliyohudumu.
Uzoefu pia kisiasa, ni jambo linalompa nguvu ya kuweza kupambana na aliyekuwa kiongozi wake katika kampeni zake za udiwani na baadaye ubunge. Heche ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Bavicha kuanzia mwaka 2011 hadi 2014, na baadaye mjumbe wa Halmashauri.
UDHAIFU
Kushindwa kutekeleza baadhi ya ahadi zake na kujiwekeza zaidi kwenye siasa za kitaifa. Hili linatajwa kuwa mojawapo ya udhaifu wake.
Mwalimu Moses Magige ambaye anafundisha moja ya shule katika jimbo hilo, anataja baadhi ya ahadi hizo kuwa ni ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kutoka Nyamwaga – Mriba – Ibaso, uchimbaji wa visima vya maji katika vijiji vya Mriba, Jibaso, Tegonga, Nyasincha. Umeme katika vijiji vya Kenyamosabi, Masurura na Masanga.
Mwalimu Moses anaongeza kuwa, Heche pia aliahidi ujenzi wa madarasa katika shule za Masurura, Kalegatonga.
“Sasa hivi tunamuona analalamika kuwa amepiga sana kelele bungeni ili ahadi hizi zitekelezwe, lakini hazijatekelezwa, sasa shida inayokuja kwake ni kwamba, wananchi wanataka- outcome (matokeo) siyo malalamiko”.
Jazba vilevile ni mojawapo ya udhaifu wake kiongozi huyu kijana. Kama ilivyo kwa Waitara, Heche ni mmojawapo ya viongozi wenye hulka ya jazba mbali ya kuwa na ukali.
Katika moja ya mahojiano, aliulizwa iwapo taswira hiyo ya kuwa kiongozi wa haiba ya ‘ngumi mkononi’, na kufafanua kuwa si kweli kwani uzungumzaji wa ukali hutokea kulingana na mazingira ya eneo husika.
HIVI NDIVYO WANAVYOTAMBIANA
Kwa upande wake Waitara amemtambia vilivyo Heche na kila mkutano wake lazima ‘amchape’. Hivi karibuni alieleza kuwa, Heche ni sawa na kinyago alichokichonga mwenyewe, hivyo atakibomoa mwenyewe. Anamsubiri amshikishe adabu jimboni.
Wakati Waitara akijigamba hivyo, kwa upande wake Heche anasema anamsubiri kwenye sanduku la kura kwa kuwa aliyofanya, wananchi ndiyo mashahidi.
Heche anasema Waitara hana uwezo wala vigezo vya kumshinda katika sanduku la kura kutokana na tabia yake ya usaliti na kutelekeza wananchi wa Ukonga. Hivyo anamshauri kuanza kujifikiria kazi nyingine ya kufanya au kusubiria uteuzi wa nafasi 10 za upendeleo kutoka kwa rais.
“Ndani ya miaka mitano nimefanikiwa kujenga vituo vya afya tisa na hospitali moja inayomilikiwa na halmashauri, ipo pale Nyamwaga, kila shule ya sekondari na msingi nimepeleka saruji, mabati, mbao na misaada kadhaa ambayo yote ililenga kuondoa changamoto kwa wanafunzi wetu, wananchi wa Tarime Vijijini wote ni mashahidi kwa namna ninavyowapambania wananchi, sasa nashangaa mtu mmoja anakuja kusema yeye anafaa wakati aliwatelekeza wananchi wa Ukonga.
“Mimi nikishindwa na Waitara kwa haki nitakubali kusaini na kwenda nyumbani kufanya shughuli zangu lakini kama kutakuwa na mtu anajaribu kuchezea kura zangu, nipo tayari kuimbiwa wimbo wa parapanda italia, hili nalisema kwa uwazi kabisa maana nimeanza kusikia watendaji wanajigamba kwamba hawawezi kuwatangaza madiwani wa upinzani hata kama wameshinda, anasema Heche.
NA GABRIEL MUSHI
Toa maoni yako kupitia 0715126577
