TAARIFA za ndani za klabu ya West Ham United maarufu kama ‘Wagonga Nyundo wa London’, zinaeleza kuwa meneja wa timu hiyo, David Moyes, sambamba na wachezaji wawili, wameambukizwa virusi vya corona vinavyosababisha ugonjwa wa COVID-19.
Mapema asubuhi ya leo West Ham wameutaarifu umma kuwa mchezaji Issa Diop sambamba na Josh Cullen pamoja na Meneja Moyes walibainika kuambukizwa COVID-19 baada ya vipimo kufanyika katika kujiandaa na mzunguko wa tatu wa kombe la Carabao dhidi ya Hull City hapo jana.
Timu ya madaktari walitaarifa kuhusu matokeo ya vipimo wakati timu hiyo ilipokuwa katika uwanja wa mazoezi wa London kujiandaa na mchezo wa Jumanne jioni katika mzunguko wa tatu wa Michuano ya Carabao dhidi ya Hull City. Meneja sambamba na wachezaji hao tayari wameshaachana na kambi na kurejea nyumbani.
Mwisho timu hiyo imewatakia kupona haraka, hata hivyo Meneja Msaidizi, Alan Irvin, alikaimu majukumu ya timu hiyo na matokeo ya mchezo wa jana usiku West Ham waliibuka na ushindi wa 5-1, Sebastien Haller na Andriy Yarmolenko wamefunga mabao mawili kila mmoja wakati Robert Snodgrass akitamatisha karamu hiyo ya magoli.
Irvin amenukuliwa akisema; “Majira ya saa 12:20 jioni punde tulipokea taarifa kutoka kwa daktari wetu na kutueleza kuwa watu wetu watatu muhimu katika timu wameambukizwa COVID-19 ambao ni Meneja na wachezaji wawili.”
