MGOMBEA ubunge wa Jimbo la Ubungo kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Boniface Jacob, amesema kuwa uongozi wa chama chake katika ngazi ya jimbo kwa miaka 10 pamoja na umeya aliokuwa akiuhudumu wamefanya kazi kubwa ya kuwaletea maji wananchi wa Ubungo.
Boniface ambaye alikuwa Meya wa Ubungo amesema hayo leo Ijumaa, Septemba 25, 2020 wakati akizungumza katika Kipindi cha Front Page cha +255 Global Radio na kusema:
“Maji Ubungo siyo kero na kama maji Ubungo ni kero basi wananchi wa Ubungo waninyime kura. Chadema tumetengeza barabara nyingi za lami Ubungo, hizi barabara za DMDP tumesaini sisi na zinatekelezwa ikiwemo ya Sinza-Mori mpaka kwa Askofu Kakobe.
“Sisi tumezaliwa Ubungo, maji yalikuwa yanapatikana sehemu tatu tu, Lufungila-Mwenge, Chuo Kikuu na Kimama Tangini. Ubungo haikuwahi kuwa na bomba la maji, tulikuwa tunapanga ndoo Mwenge mpaka Mlimani City, foleni ukienda saa 10 umechelewa.
“Mnyika alipoingia madarakani tukasambaza mabomba ya maji yaliyoitwa ya Kichina, nyumba zote mpaka za chumba kimoja. Ikaja shida nyingine; maji hayatoki kwenye maeneo ya miinuko kama Kimara, tukaleta mradi wa kupandisha maji kwenye miinuko,” alisisitiza mgombea huyo.
