WAGOMBEA ubunge wa Jimbo la Ubungo, Boniface Jacob (Chadema) na Prof. Kitila Mkumbo (CCM) ambao wanachuana vikali katika kinyang’anyiro hicho cha uchaguzi mkuu ujao wa Oktoba 28, 2020 wamekutana pamoja katika kipindi cha Front Page kinachoruka kupitia Global Radio kueleza sera zao kuelekea uchaguzi huo.
Wakizungumza katika kipindi hicho kilichoruka leo asubuhi LIVE kupitia +255 Global Radio na Global TV Online, mazungumzo yao yalikuwa hivi:
Profesa Kitila Mkumbo, Chadema aliyeongea LIVE kwa njia ya simu alisema:
“Kero kubwa wanayosema wananchi wa Ubungo ni ubovu wa barabara, tutaishawishi Serikali Kuu iongeze bajeti ya TARURA kwa ajili ya barabara zinazokwenda mitaani, kutenga asilimia 2-5 (kwa mwaka Tsh bil. 1) ziende kwenye barabara, mfuko wa jimbo ukahudumie barabara.
“Kitila Mkumbo ni Mnyiramba kutoka Singida, Boniface Jacob ni Mnyakyusa kutoka Mbeya, tupo watu milioni sita Dar, Wazaramo hawazidi milioni moja, wanaokaa hapa wametoka sehemu tofauti, hiyo siyo hoja tulishatoka kwenye ukabila na kubaguana.
“Nimekaa Ubungo kwa nusu ya umri wangu, nimeingia Dar mwaka 1992 nikiwa Sekondari ya Pugu, mwaka 1995 nikaingia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam sijawahi kutoka Dar, nimejenga Kilimahewa, Goba na Mbweni, ninaifahamu vizuri Ubungo.
“Kwa Ubungo CCM tumefanya kazi kubwa kwenye sekta ya maji, hao Chadema barabara zilikuwa chini ya manispaa wameshindwa, mitaro michafu, masoko machafu, huyo Boniface Jacob alikuwa Meya lakini ameshindwa,” alisema Prof. Kitila.
Aidha, kwa upande wake, Boniface Jacob aliyekuwa studio moja kwa moja alisema:
“Suala la uenyeji, Prof. Kitila amekuja Dar es Salaam, mimi nimezaliwa Ubungo-Maziwa, ninachosema wala si ubaguzi ila profesa achukue muda wa miaka mitano kufahamu Ubungo kwanza ndipo agombee ubunge.
“Huwezi kuishi UDSM ukajua shida za mtaani, kule wana lami kila kona, hawana shida ya umeme wala maji, wana baa zao, Mlimani Primary ina walimu wa kutosha mpaka wanafundisha Kichina, Prof. Kitila alijifungia Chuo Kikuu atazijuaje shida za Mburahati?
“UDSM unatoka darasani mpaka unakwenda kulala haukanyagi lami, Prof. Kitila amejifungia kama gerezani, hata msiba ukitokea Ubungo-Mataa hawezi kujua sababu jamii ya Chuo Kikuu na huku uraiani ni vitu viwili tofauti.”
