
Bosi wa Lebo ya Miziki ya Miziki na B-Band, Banana Zorro, (Tompo) amefanya ziara katika studio za +255 Global Radio leo Oktoba 02-2020 na kutambulisha mkwaju wake mpya wa Aiyaya kupitia Bongo 255 inayoongozwa na Stewart George, Darboi na mtoto mzuri Noreen.

Banana alitinga katika studio za Global Radio akiwa na msanii mrembo Ashura Kitenge ambaye amempa shavu kwenye mdundo huo ambao una mahadhi ya Kibongo Fleva na una maudhui ya mapenzi.

Akitambulisha mkwaju huo, Banana alisema ameamua kufanya muziki wa kitofauti ambao wasanii wengi wa sasa hawaimbi pamoja na kuleta utofauti sokoni na kujaribu kuwaonyesha vijana namna ambavyo nyimbo za mapenzi zinaimbwa.
“Wasanii wengi wa siku hizi hawajui kabisa kuimba nyimbo za mapenzi, nyimbo zao hazizungumzii mapenzi bali zinahamasisha watu kufanya mapenzi kitu ambacho siyo sawa.
“Kwahiyo Aiyaya imekuja kutoa darasa la namna gani mikwaju ya Bongo Fleva inatakiwa kuimbwa. Huu ndiyo muziki ambao unatakiwa sokoni, utamsikia Ashura vizuri na hata mimi Tompo utasikia namna ambavyo namlilia mtoto mzuri humo ndani,” alisema Banana.
Stori na Na Issa Liponda