×

 Asanteni wana-Buchosa Hakika Mmeonesha Upendo Mkubwa!

KWANZA kabisa nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kuifikia tena siku hii ya leo, pili niwashukuru wananchi wa Buchosa, ndugu zangu, mama zangu, kaka zangu na dada zangu, nina furaha moyoni kusema niwashukuru sana.

 

Hakika nimeamini kwamba, kweli mnajua kunitoa machozi. Kwa sababu katika uzinduzi wa kampeni zangu nilipofika pale uwanjani nilipoona upendo wenu kwa wingi ule, mlinifanya nitoe tena machozi, mlinifanyia ule mchezo wenu.

 

Hakika mmenionesha upendo mkubwa sana katika maisha yangu. Nichukue nafasi hii niwashukuru sana kwa sababu mlivyokuja kwa wingi licha ya kwamba mvua ilikuwa inanyesha, lakini watu bado mliendelea kujaa uwanjani.

 

Sina la kusema zaidi ya kumuomba Mungu Baba wa Mbinguni awabariki na kuwalipa kwa upendo wenu. Ndugu zangu, napenda pia kuishukuru familia yangu, mke wangu na watoto wangu kwa upendo wanaoendelea kunionesha licha ya changamoto mbalimbali, lakini pia niwashukuru wanachama wa CCM ambao kwa kauli moja waliamua mimi niwe mwakilishi wa wana-Buchosa bungeni.

 

Hakika ulikuwa mchakato mrefu, wenye mateso, kwa wale walioshiriki watajua kuwa ulikuwa mchakato mrefu, mgumu na wenye mateso, nawashukuru sana watia nia wote 34 tulioshindana pamoja. Ninawashukuru waliofika katika uzinduzi ule na ambao hawakufika.

Lakini kipekee kabisa kutoka ndani ya moyo wangu, nichukue nafasi hii kumshukuru sana Dk Charles Tizeba. Huyu ni mtu muungwana ni mtu mwema alichokifanya kufika katika uzinduzi wa kampeni zangu siyo kitu rahisi sana. Katika uchaguzi kuna kushindwa na kushinda na kwa kweli mimi niliwahi kushindwa 2010 naelewa kushindwa ni nini.

 

Alichokifanya Dk Tizeba kimenipa moyo kimenifurahisha, nataka niwaambie wana Buchosa, Dk Tizeba alikuwa mshindani wangu sana, tulipambana kabisa. Lakini mwisho wa siku amekubali na ameamua kuniunga mkono, hiki siyo kitu kidogo, Dk Tizeba nakushukuru sana.

 

Napenda kuwahakikishia wana-Buchosa wote, nitafanya kazi na mtu yeyote, mtu wa kwanza ambaye nitafanya naye ni Dk Tizeba ili kuleta maendeleo ya eneo letu. Kwa sababu hatuwezi kuendeleza migawanyiko hii kwa sababu inatuchelewesha. Napenda kuwaomba Watanzania wote wenye mapenzi mema, tuendelee kuhudhuria kampeni za CCM, kuwasikiliza wagombea wetu akiwamo Mgombea urais, Dk John Magufuli.

Moyoni mwangu bado nina imani kubwa na Rais John Magufuli, kwa mambo aliyoyafanya na ambayo Watanzania mmeyashuhudia kwa macho yenu ndani ya miaka mitano, nchi yetu imetoka kwenye uchumi wa chini kuja kwenye uchumi wa kati ndani ya miaka mitano, Je, miaka mitano ijayo nchi itakuwa wapi?

 

Napenda kuwaambia Watanzania wenzangu, uchaguzi ni uamuzi, uchaguzi ni busara ya kuamua nani unamkabidhi hatima ya maisha yako, ni uamuzi mkubwa si mdogo, Hatuchagui chama, hatuchagui mtu tunachagua maisha yetu. Kwa hiyo ni lazima kuangalia kabisa unamchagua nani kwa sababu ndiye unamkabidhi mustakabali wa maisha yako, hili siyo jambo la majaribio.

 

Hatufanyi majaribio kwenye kuchagua viongozi. Ndugu zangu, ni lazima kuangalia mtu ambaye kweli ameonesha uaminifu na kweli tunamuamini na tukimuangalia tunasema kweli huyu atatekeleza ndoto yetu.

 

Rais Magufuli ana ndoto ya kuipeleka nchi hii kwenye Tanzania mpya ambapo kutakuwa na usawa katika kila kitu. Mtoto wa maskini katika nchi hii awe sawasawa na mtoto wa tajiri.

Mama mjamzito aliyepo kijijini apate huduma sawasawa na mama mjamzito aliyepo mjini, hiyo ndiyo Tanzania ambayo Dk Magufuli anaitaka na hiyo ndiyo Tanzania ambayo mimi ninatamani kuiona.

 

Tanzania ambayo mke wangu anapotaka kujifungua anakwenda kujifungua Aga Khan, haimaniishi kwamba kitendo cha mke wangu kwenda kujifungua pale maisha yangu ni bora sana kuliko maisha ya mama aliyeko katika Kijiji cha Nyehunge au Kalyebezo, Tanzania lazima tuwe na usawa.

 

Nataka kuiona Tanzania ambayo shule anayosoma mwanangu apate elimu sawasawa na mtoto ambaye yupo Kijiji cha Milundikwa, tuwe na usawa ili katika nchi hii kila mtu awe na nafasi ileile sawa na mtu mwingine.

 

Nchi yetu hapa tulipofika ni juhudi za Rais Magufuli, sasa hivi mikopo imeongezeka kwa watoto wetu waliopo vyuo kikuu. Elimu yetu sasa hivi ni bure, ndugu zangu ni nini zaidi tunachokitaka? Tazama umeme, tazama reli, tazama ndege, yote haya ni dalili ya kwamba mtu huyu ana nia njema na Taifa letu.

 

Rais wetu ana nia njema na nchi yetu, tuendelee kumuamini kwa miaka mingine mitano. Sioni mtu mwingine wa kumkabidhi Taifa hili. Nasema haya siyo kwamba nadharau wengine, hapana, naangalia historia ya mtu ili niweze kufanya maamuzi.

 

Unapofanya maamuzi ndugu zangu angalia historia ya mtu, huyu mtu amefanya nini huko alikotoka, inakusaidia kufanya maamuzi yako leo. Mgombea huyu ni mwaminifu, mgombea huyu ni mtiifu, anastahili kuaminiwa hana tamaa, amefanya vitu vingi vya kuthibitisha hana tamaa.

 

Angekuwa na tamaa Kampuni ya Airtel India ambao wamekuja kulipa fedha nyingi, kwenye migodi makampuni ya wazungu yamebanwa yamelipa fedha nyingi angekuwa ni mtu mwenye tamaa angesema niwekee fedha hizi kwenye akaunti sehemu fulani.

 

Tunafahamu viongozi wa Afrika wanavyofanya, wanaingia madarakani na kujitajirisha. John Magufuli ni picha halisi ya Mwalimu Nyerere na viongozi wetu wengine waliotutangulia. Ninawaomba Watanzania wenzake na Wana-Buchosa, tumuunge mkono Rais Magufuli kwenye uchaguzi huu.

 

Tumpe kura nyingi za ndiyo, rais wetu, wabunge nikiwamo mimi katika jimbo hili la Buchosa na pia madiwani wetu, haya yakifanya napenda kuwahakikishia Tanzania itaenda mbele kwa kasi. Ndugu zangu, unayo thamani kubwa usijidharau. Kura yako moja uliyoishika mkononi itakuletea mabadiliko makubwa ya nchi yako. Usijipuuze ukajiona haina thamani.

 

Ungekuwa huna thamani sisi wanasiasa, tusingekufuata kijijini kukuomba kura, kwa nini tumeacha kila kitu tumekuja kwako. Ni kwa sababu unayo thamani, fanya maamuzi sahihi sasa kwa kura yako moja uliyoishika. Nyanyuka nenda ukapige kura.

 

Ndugu Wana-Buchosa, ninafahamu tunazo changamoto nyingi sana za barabara, maji, huduma za afya na elimu. Tuna eneo kubwa sana la kilomita za mraba zaidi ya 6000, lakini hatuna chuo hata kimoja cha ufundi, tuna shule ya kidato cha tano na sita moja tu, sikubaliani na jambo hii.

 

Mambo haya ni baadhi ya mambo ambayo yamenisukuma niamue kwamba nitaacha kila kitu nikawatumikie watu hawa ili nioneshe kwa vitendo uongozi maana yake ni nini, maendeleo huja kwa uongozi bora, kama hakuna uongozi bora hapawezi kuwa na maendeleo.

 

Ndiyo maana nimekuja kwenu na mmenipokea mmenipa kura nyingi ambazo kwa kweli sikuzitarajia, napenda kuwahakikishia kuwa tutafanya kazi pamoja, tuashirikiana pamoja, tutapambana pamoja hatutaiachia Serikali kila kitu.

 

Ndugu zangu, Serikali haiwezi kutatua matatizo yote tuliyonayo, haiwezi kuja kushusha neti ndani ya nyumba yako watoto walale, haiwezi kuja kusimamia watoto wako wafanye homework, lakini wewe mzazi utaamua watoto wako wafanya homework kwa sababu kwa kufanya hivyo, unajenga nchi yako. Taifa letu Tanzania haijengwi na watu wanaokaa mbele katika kurasa za magazeti.

 

Inajengwa na watu wadogowadogo ambao hata habari zao haziandikwi na watu hao ni sisi Watanzania. Nimalizie kwa kuwaomba ndugu zangu Wana-Buchosa, mnipe kura za kutosha ifikapo Oktoba 28, mwaka huu, ninawahakikishia kutekeleza haya yote kwa kushirikiana nanyi.

Mungu ibariki Tanzania!

 

Leave a Comment