
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. John Mongella ameitaka Benki ya NCBA kusaidia kwenye pamba, uvuvi, madini, viwanda, nishati na ufugaji.
NCBA Bank Tanzania Limited ilisheherekea hatua nyingine ya kihistoria ya ujio wake nchini kwa kuzindua matawi mengine mawili mapya mkoani Mwanza mnamo tarehe 2 Oktoba.
Matawi hayo yanapatikana Plot No 5, Barabara ya Nyerere na Jengo la Kauma lililopo Barabara ya Kenyatta.
Hafla hii ni kati ya sherehe zinazoendelea za ujio wa Benki ya NCBA ambayo ni muunganiko wa hiari kati ya NIC Bank (T) Limited na CBA Bank (T) Limited ambapo huduma rasmi za taasisi hii mpya zilianza tarehe 8 Julai 2020 baada ya idhini ya Benki Kuu ya Tanzania.
Uzinduzi huo ulianza kwa matembezi yenye nderemo na shangwe wakitamka kauli yao mbiu iitwayo GOR FOR IT kutoka kwa wafanyakazi wa NCBA kwenye mitaa na barabara ya jiji la Mwanza kutoka tawi lao lililopo kitalu namba 5, Barabara ya Nyerere hadi Jengo la Kauma lililopo Barabara ya Kenyatta na baadae kukafanyika hafla ya jioni kuhitimisha uzinduzi huo.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza aliyekuwa Mgeni Rasmi katika matukio yote mawili alitoa wito wake kwa Benki ya NCBA kwa kuwekeza kwenye sekta muhimu za uchumi kwenye mkoa wa Mwanza wenye idadi ya watu takribani milioni moja. Alikaririwa akisema;
“Tunajivunia rasilimali watu kwani Mwanza ni mji wa pili kwa ukubwa hapa nchini Tanzania wenye takriban watu milioni 1.
“Ni moja wapo ya miji inayokuwa kwa kasi kubwa zaidi kutokana na fursa, rasilimali na shughuli za kiuchumi katika sekta zote nilizozitaja, iwe madini, kilimo, mifugo, uvuvi na viwanda’.
“Mwanza inategemea sana shughuli ya uvuvi, ambayo inaongoza kwa mapato ya fedha ikiwemo zile za kigeni.
“Jiji hili lina viwanda 13 vya kusindika samaki vyenye uwezo wa kusindika karibu tani 1,065 za samaki kwa siku, hivyo kutoa mchango mkubwa unaoimarisha uchumi wa mkoa huu kwa kutoa ajira mbali mbali kwa wananchi”. Alisema Mkuu wa Mkoa.

Mhe. Mongella aliendelea kusisitiza kuhusu umuhimu wa kusaidia maendeleo ya sekta ya biashara kwa viwanda vidogo, vya kati na vikubwa. Mkuu huyo wa mkoa ameendelea kusema;
“Ni imani yetu kuwa Benki ya NCBA kama taasisi ya fedha itakuwa moja ya washirika bora watakaowezesha wafanyabiashara wadogo, wa kati na wakubwa kusonga mbele katika hatua mpya ya maendeleo na kukuza pato la Taifa”.
Mkurugenzi Mkuu na Afisa Mkuu Mtendaji wa Benki ya NCBA, Bi Margaret Karume aliwahakikishia wadau, wageni na wateja kuwa benki hiyo inatoa huduma bora za kiwango cha kimataifa mahali popote walipo na kuongeza;
“Ninayofuraha ya kuwahakikishia wateja wetu wote kuwa wapo huru kutembelea tawi lolote lile la NCBA Bank ili kupata huduma zilizo bora kwa kiwango cha kimaitaifa, iwe hapa Mwanza ama katika miji mingine au Visiwani Zanzibar.

“Pia kufuatia muunganiko wetu, wateja wana uhuru na urahisi wa kutumia mashine yoyote ile ya ATM yenye nembo ya NCBA Bank ukiwa Mwanza, Arusha, Zanzibar, Dar es salaam ama katika nchi jirani za Kenya, Uganda, Rwanda, na Ivory Coast”. Alisema Bi. Margret Karume.
Bi.Margaret Karume, alimshukuru Mkuu wa Mkoa pamoja na waheshimiwa wageni waalikwa kwa utayari wao wa kuiunga mkono Benki ya NCBA. Margaret Karume alisisitiza umuhimu kwa Benki ya NCBA kuunga mkono mageuzi ya kiuchumi ya Mkoa wa Mwanza na Taifa kwa ujumla.
Amesema Benki ya NCBA inaleta kwa pamoja ubora wa dunia mbili. Kuchanganya nguvu za taasisi mbili za awali zilizofanyika benki ya NCBA kuwa benki kubwa na yenye nguvu kifedha, yenye utaalam na uwezo mkubwa unaowaweka wateja wake mstari wa mbele katika safari yao ya mafanikio.